Na:Rosetha
Gange
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe.Ng’wilabuzu Ludigija leo tarehe
1/7/2021 ameiongoza timu ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Ilala na kufanya
ziara ya kushitukiza kwenye kiwanda bubu
kinachojishughulisha utengenezaji wa sabuni na usagaji wa Salfa
inayodaiwa kutumika kuulia wadudu kwenye mashamba ya mikorosho.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija akiongoza timu ya wataalamu waliofika kukagua kiwanda hicho |
Kiwanda hicho kinachoendeshwa bila kibali wala leseni yoyote kutoka katika mamlaka husika kinamilikiwa na Bw.Dunia Amrani Kitumbi kipo Kata ya Pugu mtaa wa Kinyamwezi katika Halmashauri ya jiji la Dar es salaam kinadaiwa kuharibu mazingira na kuhatarisha afya za wakazi wa maeneo hayo.
Akiongea kuhusiana na Kiwanda
hicho, Mhe.Ludigija amesema Salfa inayosagwa katika kiwanda hicho haifai kwa
matumizi yaliyokusudiwa (kuulia wadudu kwenye mashamba ya korosho) kwani badala ya kuua wadudu yanaua miche ya
mikorosho hivyo wanawaibia wananchi wa mikoa ya Lindi,Mtwara na maeneo mengine
ambako malighafi hiyo inapelekwa.Vilevile kuendesha shughuli yoyote bila kibali
wala leseni kutoka katika mamlaka zinazohusika ni kinyume na sheria pia ni
kuiibia mapato Serikali.
Mhe.Ludigija anasema,
“Salfa ni kemikali hatarishi kwa afya za viumbe hai yaani mimea na
wanyama wakiwemo binadamu na mazingira yanayomzunguka.Vilevile Salfa ina uwezo
wa kushika moto kirahisi, hivyo kufanya shughuli hizi katika eneo hili kunaweza
kusababisha madhara makubwa kwa wakazi wanaokizunguka kiwanda hiki.”
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija (kulia) akimueleza jambo mmiliki wa kiwanda hicho Bw.Dunia Amrani |
Akiongelea tukio hilo Msimamizi wa Ukaguzi wa kanda ya Mashariki kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali amesema kuwa wao kama wasimamizi wa sheria ya udhibiti na usimamizi wa kemikali za majumbani na viwandani walifika katika eneo hilo na kukuta kiwanda hicho kisicho rasmi kinatunza kemikali hatarishi na kinafanya shughuli zake bila kusajiliwa na Mkemia mkuu,hivyo ni kosa kwani wamekiuka sheria ya udhibiti.
Mhe.Ludigija ameunda kamati maalum
ya kuchunguza kiwanda hicho kwa kina ili kujua Salfa hiyo inamilikiwa na watu
gani,inatoka wapi na inakwenda wapi na inatumika kwa matumizi gani baada ya
kuchakatwa.Pia kufanya uchunguzi kama wamiliki wa mzigo huo wana vibali vya
kumiliki mzigo huo.
Sehemu ya shehena ya kemikali aina ya Sulphur iliyokamtwa |
Kwa sasa Kiwanda hicho kilichohifadhi Salfa inayokadiriwa kuwa na zaidi ya tani mbili kimefungwa na mmiliki wake anashikiliwa wakati uchunguzi ukiendelea kufanyika huku Mhe. Ludigija akitoa rai kwa wananchi wengine wanaofanya shughuli za namna hiyo waache kwani wanachafua mazingira na wanahatarisha afya za wananchi na kudidimiza uchumi wa Taifa kwa ujumla.Vilevile amewataka kufuata taratibu za kisheria wanapotaka kufanya biashara na sio kufanya kinyemela ili kukwepa kodi kwani kodi inasaidia katika ujenzi wa barabara,Zahanati, kununua dawa, Ujenzi wa shule na shughuli nyingine nyingi za kimaendeleo.