Ushirikiano baina ya Jiji la DSM na Hamburg waendelea kuimarika

 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Leo tarehe 9 Novemba,2022 imepokea wageni kutoka Jiji la Hamburg ,Ujerumani waliokuja kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali hasa masuala ya Ustawi wa Jamii na kufanya Utalii katika vivutio vinavyolipamba Jiji la Dar es Salaam na maeneo jirani.

Akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini Bi.Tabu Shaibu amewakaribisha wageni hao na kuwaomba waulinde na kuuendeleze ushirikiano huo kwani una manufaa makubwa kwa pande zote mbili yaani Ujerumani na Tanzania.



"Tuulinde na kuuendeleza ushirikiano huu kwani kupitia muungano wetu sote tunapata maarifa mapya kupitia programu tofauti tofauti tunazozifanya." Amesema Bi.Tabu Shaibu

Miongoni mwa maeneo ambayo Miji ya Hamburg na Dar es Salaam hushirikiana ni katika Upande wa Mazingira ambapo pande zote mbili zilikubaliana kutoa elimu kwa Jamii juu ya namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, upangaji wa Miji, masuala ya afya, Elimu, Ustawi wa Jamii, kukuza Utalii katika Jiji la Dar es Salaam na Biashara kwa kutumia Bandari ya Dar es Salaam.

Wageni hao wamekuwepo katika Jiji la Dar es Salaam kwa muda wawiki mbili sasa, kufuatia programu yao inayoitwa DAKA yenye wataalamu wa Mazingira, wanaharakati wa maendeleo,wataalamu wa afya na wataalamu wa mambo ya Ustawi wa Jamii ambapo lengo la programu yao ni kubadilishana uzoefu katika masuala hayo.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi