Maafisa Lishe kutoka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wameendelea kutoa elimu na kuhamasisha wananchi juu ya matumizi sahihi na mpangilio bora wa vyakula ili kuimarisha afya na kuepuka magonjwa yanayoweza kuwapata mara kwa mara.
Elimu hiyo imetolewa Leo tarehe 31 Agosti, 2023 katika siku ya Afya na Lishe kwa Kata ya Jangwani kwenye Mkutano uliowashirikisha Maafisa Lishe kutoka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Viongozi wa Kata na Mitaa, Wananchi na wadau mbalimbali wa Afya pamoja Lishe.
Mbali na kufundisha kuhusu mpangilio bora wa mlo kamili somo lililofundishwa na Bi. Neema Mwakasege, wananchi pia walipata fursa ya kufundishwa namna ya kuandaa chakula cha mtoto mwenye umri wa kuanzia miezi sita na kuendelea ambapo Bi. Neema Manyama aliandaa uji wenye makundi matatu ya vyakula ambayo ni nafaka, maziwa pamoja na sukari.
Aidha, suala la lishe bora linakwenda sambamba na usafi pamoja na usalama wa chakula kuanzia shambani kinapotoka mpaka muda wa kuliwa. Bi. Safiona Mdee ambaye ni Afisa Lishe wa Kata ya Jangwani amesema kuwa ili chakula kiwe Safi na salama lazima taratibu na kanuni za usafi wa chakula zifuatwe.
"Ni vyema kuzingatia kanuni na taratibu za usafi na usalama wa vyakula hupita maeneo mbalimbali ambayo yanaweza kuwa sio salama kabla ya kumfikia mlaji mfano sokoni ambapo uhifadhi wake unaweza kuwa si salama au shambani ambapo nafaka hupulizwa dawa za kuua wadudu ili zisiharibike haraka hivyo kufanya vyakula hivyo kuwa hatarishi kutumiwa moja kwa moja na mlaji bila kuchukua tahadhari yoyote." Amesema Bi. Mdee
Kwa upande wa wananchi waliohudhuria mkutano huo wamewashukuru wataalamu kwa masomo mazuri waliyoyatoa kwao na kuwafanya wajifunze mambo mengi waliyokuwa hawayafahamu kuhusu lishe bora na kutoa wito kwa wananchi wa maeneo mengine kujitokeza kwa wingi pale Maafisa Lishe wanapowatembelea katika mitaa yao.