Halmshauri ya Jiji la DSM yafanya mafunzo na maonesho ya mama lishe

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii kwa kushirikiana na Benki ya NMB Leo tarehe 22 Machi, 2024 imefanya mafunzo na maonyesho kwa mama lishe wa Wilaya ya ilala, katika viwanja vya Karimjee yenye kaulimbiu ya “Wekeza katika nishati safi ya kupikia na mazingira“ yaliyolenga kuwajengea uwezo katika uandaaji wa chakula salama kwa walaji na kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika jitihada zake za kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala ya gesi lengo ikiwa ni utunzaji wa mazingira.


Akiongea na mama lishe katika mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo amesema "Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekua mstari ya mbele katika kusisitiza swala zima la utunzaji wa mazingira kwa kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala ya gesi hivyo tumuunge mkono katika jambo hili kwa kuacha matumizi ya kuni na mkaa. Pia tutunze na kuboresha mazingira tunayofanyia biashara kwa kuyafanyia usafi kwa usalama wenu na wateja wenu."


Sambamba na hilo Mhe. Mpogolo amewashukuru mama lishe na baba lishe kwa kazi ngumu na nzuri wanayoifanya ya kuwahudumia wananchi wa Ilala “Ninyi ni watu muhimu sana katika Wilaya yetu, wananchi wanaokuja mjini kwaajili ya kujipatia riziki nyakati za mchana ni wengi na wanahitaji chakula wanapokua kwenye majukumu yao, asilimia kubwa ninyi ndio mnaowahudumia hivyo niwapongeze kwa kazi nzuri na ngumu ya kuwahudumia wananchi."


Aidha, Afisa Lishe wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Bi. Neema Mwakasege amewasisitiza mama lishe kupika vyakula vyao kwa kuzingatia Lishe Bora inayozingatia makundi 6 ya vyakula ili kuepukana na magonjwa yasioambukiza.


Mafunzo hayo yaliliambatana utoaji wa zawadi kwa mama lishe waliofanya vizuri katika swala zima la usafi na uandaaji wa chakula ili kutoa motisha kwa mama na baba lishe wengine. Zawadi zilizotolewa ni mitungi ya gesi.


Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi