RC Chalamila asikiliza na kutatua kero za wananchi wa Jimbo la Ukonga

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila leo tarehe 28 Mei, 2024 amefanya mkutano wa hadhara wenye lengo la kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa Jimbo la ukonga ambapo ameahidi kutatua changamoto zinazowakabili wananchi hao.


Akiongea na wananchi kwenye mkutano huo uliofanyika kwenye Viwanja vya Pugu, RC Chalamila amepokea changamoto mbalimbali zikiwemo za Miundombinu, masoko na migogoro ya ardhi ambapo zipo alizotatua papo kwa papo na nyingine kuzipatia utatuzi kwa kuwataka watendaji kuhakikisha wanazishughulikia.


"Niwaombe wananchi wa Jimbo la Ukonga Ili kupunguza migogoro ya ardhi na changamoto nyingine nawaasa kuchagua viongozi bora bila kujali itikadi zao za vyama, watakaoweza kumsaidia Mheshimiwa Rais kutekeleza nia aliyonayo kwa wananchi. Pia sisi viongozi tulioteuliwa na kuchaguliwa tufanye wajibu wetu kuhakikisha mambo yote yanakwenda sawa.” Amesema Mhe. Chalamila.


Awali akifungua mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo ameeleza kuwa “Nitoe shukrani zangu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr Samia Suluhu Hassan kwa kutatua kero ya miundombinu ya barabara kwa kutupatia zaidi ya Bilioni 231 kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ya mwendokasi kuhakikisha wananchi wanapata usafiri kwa urahisi. Pia nikushukuru Mkuu wa mkoa kwa kuona haja ya kuja kusikiliza kero za wananchi wa Jimbo la Ukonga na nikuhakikishie tutazingatia haki katika kutekeleza yote utakayotuagiza."


Katika ziara hiyo RC Chalamila aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Ilala , wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Wilaya,  Viongozi wa Chama wa Wilaya ya Ilala, Wataalamu kutoka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na wengine kutoka Taasisi zinazowahudumia wananchi kwa ukaribu ikiwemo Wakala wa Barabara za Vijijini na Mji (TARURA) , Wataalamu kutoka Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira (DAWASA) pamoja na wataalamu kutoka Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO).


Nae Mstahiki Meya wa Jiji la DSM Mhe. Omary Kumbilamoto ameshukuru kwa ziara hiyo ya Mkuu wa Mkoa na kupongeza juhudi anazozifanya kuhakikisha anatatua kero kwa haki bila upendeleo , na kumuhakikishia kushirikiana nae na kutekeleza yale Yote aliyowaagiza.


Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi