Waziri Mchengerwa awataka madereva bodaboda kujisajili kwenye mfumo wa kidigitali

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Maafisa usafirishaji (Madereva bodaboda na bajaji) kuhakikisha wanajisajili katika mfumo wa kidigitali (Kanzi Data) lengo likiwa ni kuwatambua madereva hao kwa urahisi zaidi na kuweza kutambua mchango wao katika maendeleo ya nchi.



Mhe. Mchengerwa ametoa wito huo leo Julai 1,2024 Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa sare (Uniform) Maalum na Mfumo wa Kidigitali (Kanzi Data) wa Madereva Bodaboda na Bajaji Mkoa wa Dar es Salaam iliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini humo.



Akizungumza wakati wa hafla hiyo Mhe. Mchengerwa, amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Ilala pamoja na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam kwa ubunifu walioufanya wa kuhakikisha wanawatambua bodaboda na bajaji wa Wilaya ya Ilala kwani ubunifu huu unawaunganisha madereva hao kuweza kushirikiana katika mambo mbalimbali ya kujenga Taifa huku akitoa Wito kwa Wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam na Nchi kwa ujumla kufanya hivyo.



Sambamba na Hilo, Mhe. Mchengerwa amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote Nchini kuhakikisha wanawalinda na kuwajali maafisa usafirishaji (madereva bajaji na bodaboda) kwa kuwatambua katika vituo vyao vya maegesho pamoja na kuhakikisha wanajisajili kwenye mfumo wa kidijitali huku akiwataka kushirikiana na Halmashauri zao kuwajengea maafisa usafirishaji hao vituo vya maegesho ambavyo vitawasaidia kujikinga na Mvua pamoja na jua.



Nipende kutoa pongezi kwa Wilaya ya Ilala kwa kuwaunganisha maafisa usafirishaji hawa kwani hafla hii inaonesha kuwajali na kuwathamini vijana hawa hivyo katika kutambua mchango wao ninaagiza Halmashauri zote Nchini kuhakikisha katika Mgawanyo wa asilimia 10% za mapato ya Halmashauri na maafisa usafirishaji hawa hawakosekani pia muache kukamata kamata ovyo zaidi mtumie Kamati za ulinzi na Usalama za Wilaya na Mikoa kutoa elimu kwa vijana hawa juu ya usalama barabarani”.

Halikadhalika, Mhe. Mchengerwa amewataka Waganga Wakuu wa Wilaya kuweka utaratibu wa kutoa mafunzo kwa maafisa usafirishaji hao ili kuepusha ajali mbalimbali ambazo zimekua zikitokea huku akiwahimiza maafisa usafirishaji hao kuweka utaratibu wa kukutana mara kwa mara kujali mambo mbalimbali ya kuwajenga kwani Serikali ya Awamu ya Sita Chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni sikivu na inawathamini sana.



Vilevile, amewaomba wadau wa maendeleo kutumia fursa hii ya sare maalum za badaboda kutangaza biashara zao kwa kuwatengenezea maafisa usafirishaji hao sare hizo na kuwapa bure kwani kupitia sare hizo wataweza kujitangaza na ukizingati vyombo hivyo vinazunguka maeneo mengi.



Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo ameeleza kuwa “Sisi kama Wilaya ya Ilala tushaanza kuwatambua bodaboda wote na tumewatengea vituo maalumu kwaajili ya maegesho kwani kuwatambua na kuwarasimisha inaleta utu na kuwajali maafisa usafirishaji hawa hivyo sisi kama Jiji la Dar es Salaam tutapokea maelekezo kwa utekelezaji na tunaahidi kuwapanga maafisa usafirishaji hawa katika maeneo maalumu lengo likiwa ni kuunga Mkono Juhudi za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutunza mazingira na kuhakikisha usalama wa kila mwananchi hivyo sisi tutakwenda kuwalinda na kuwatetea bodaboda na bajaji kwenye changamoto zao ili kuwa sehemu ya Mafanikio ya Nchi yetu, pia tutahakikisha asilimia 10% ya mapato ya maegesho yatakwenda kwenye Saccoss yao lengo likiwa ni kuhakikisha vijana hawa wanapata maisha bora.



Vilevile Mhe. Mpogolo amewataka madereva hao kutii sheria za barabarani ili kuepuka ajali za mara kwa mara bila kusahau kuvaa sare maalumu kwani takwimu zinaonyesha katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Kitengo cha mifupa (MOI) takribani wagonjwa 5900 ya wagonjwa wote ni ajali za bodaboda hivyo ili kuepuka ongezeko hili Wilaya ya Ilala ikaona ni vyema kuanzishwa kwa Sare maalumu na mfumo wa kidijitali kwa vijana hao hii itawatambua madereva hawa kwa uharaka zaidi na Jiji la Dar es Salam litakua linapendeza na ajali zitaepukika.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Ilala pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kuwaunganisha bodaboda na bajaji hao huku akitoa wito kwa Halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam kuwekeza zaidi kwenye kutoa elimu kwa maafisa usafirishaji hao na sio kuwakandamiza kwa ushuru wa maegesho yasiyo rasmi (Wrong Parking).



Aidha Mhe. Chalamila aliendelea kusema “Tutaona ni namna gani ya kuwasaidia madereva hawa katika kupunguza gharama za tiba kwa madereva wanaopata ajali na kupelekwa MOI ila niwatake madereva bajaji na bodaboda kuwa mabalozi nyie wenyewe kwa kujenga ustaarabu katika kuendesha vyombo vya moto pamoha na kutii sheria za barabarani ili kuepukana na ajali zisizo za lazima.



Kwa upande wake Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (ZTO), Kamishna Msaidizi wa Polisi, ACP. William Mkonda amewaasa madereva bodaboda kuvaa kofia ngumu pamoja na kutii sheria za barabarani kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia kujiepusha na ajali za mara kwa mara zisizo za lazima.



Akitoa shukrani zake kwa niaba ya maafisa usafirishaji (bodaboda/bajaji), Naibu Katibu wa Shirikisho la bodaboda na bajaji Tanzania ambaye pia ni Katibu wa bodaboda na bajaji Mkoa wa Arusha Bw. Hakim Msemo ameeleza kuwa wao kama maafisa usafirishaji watatii sheria bila shuruti pamoja na kutekeleza yote waliyoelekezwa ikiwemo kuvalia sare maalumu na kujisajili katika mfumo wa Kidigitali (Kanzi Data) wa madereva bodaboda na bajaji kwani imani yao ni kuhakikisha vifo vya ajali za bodaboda vinapungua au kutokomea kabisa kama ilivyo kwa Nchi ya Uganda huku akiiomba Serikali kuwafungulia Sacoss kwa ajili ya kujiwekeza maafisa usafirishaji ambayo itawasaidia katika kukabiliana na changamoto za maisha.


Aidha, muonekano wa Sare Maalumu yenye namba ya usajili katika kanzi data utasaidia kuthibiti vitendo vya uhalifu, kupunguza ajali za barabarani pamoja na kupunguza upotevu wa mapato ya Serikali kupitia malipo ya leseni za udereva, leseni za biashara na Maegesho.



Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi