Na:
Hashim Jumbe
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya
Ilala, Ndugu Isaya Mngurumi amekutana na Wafanyabiashara ndogo ndogo
maarufu kama Wamachinga kutoka mitaa ya Kariakoo na kujadiliana changamoto mbalimbali
wanazokabiliana nazo Wafanyabiashara hao na namna ya kuziondosha changamoto
hizo.
Katika awamu ya pili ya majadiliano hayo, Mkurugenzi
wa Manispaa ya Ilala alieleza mapendekezo ya mitaa itakayotumika kwa kufanyia
biashara ndogo ndogo za Wamachinga pamoja na muda maalum wa kufanya biashara
hizo, kama tiba ya kuondosha misongamano katika maeneo ya katikati ya Mji.
Mitaa iliyopendekezwa kutumika ni Kongo, Nyamwezi,
Swahili na Sikukuu ambapo Mitaa ya Aggrey na Mkunguni haitatumika kwa biashara
ndogo ndogo.
Mitaa mingine ni Mchikichi, Mahiwa, Narun’gombe,
Tandamti na Pemba ambapo Mtaa wa Livingstone hautatumika kwa biashara ndogo
ndogo
Aidha, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala aliagiza Mitaa
hiyo itumike kuanzia saa 10:00 jioni hadi saa 3:00 usiku kwa siku za jumatatu
hadi ijumaa, kuanzia saa 7:00 mchana hadi saa 3:00 usiku kwa siku za jumamosi
na siku za jumapili kuanzia asubuhi hadi saa 3:00 usiku.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Ndugu Isaya Mosses Mngurumi akitoa ufafanuzi wa Mitaa itakayotumika kwa Wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama Wamachinga |
Kiongozi wa Wafanyabiashara ndogo ndogo akieleza changamoto wanazokabiliana nazo wakati wa mkutano wa pamoja na Uongozi wa Manispaa ya Ilala |
Wawakilishi wa vikundi mbalimbali vya Wamachinga waliohudhuria Mkutano wa pamoja na Viongozi wa Manispaa ya Ilala |