Na: Hashim Jumbe
Aliyekuwa Kaimu Mkuu wa Idara ya Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika Manispaa ya Ilala, Ndugu Francis Eprem Luambano kuzikwa leo kwenye makaburi ya mji wao huko Peramiho-Songea.
Marehemu Francis Eprem Luambano alifariki Dunia usiku wa kuamkia tarehe 26-01-2016 kwa kupigwa risasi na Majambazi alipokuwa akirejea nyumbani kwake maeneo ya Tabata Bima.
Aliyekuwa Afisa Ushirika Manispaa ya Ilala, Marehemu Francis Luambano akifafanua jambo wakati wa kikao kazi na wakusanya takwimu Manispaa ya Ilala |
WASIFU WA MAREHEMU FRANCIS EPREM
LUAMBANO
Marehemu Francis Eprem Luamban alizaliwa tarehe 18/08/1962 huko Songea katika Mkoa wa Ruvuma.
Alipata elimu ya Sekondari katika shule ya Sekondari ya Kigonsera kuanzia mwaka
1978 na kuhitimu kidato cha nne mwaka 1981
Baadaye alijiunga na kidato cha tano katika shule Sekondari Ihungo na
kuhitimu kidato cha sita mwaka 1984. Marehemu Francis Eprem Luambano alipata elimu
yake ya Stashahada ya Usimamizi wa masuala ya Ushirika katika chuo cha Ushirika
Moshi kati ya mwaka 1985 na 1987.
Tarehe
21/08/1987 aliajiriwa kwenye utumishi wa Umma katika Halmashauri ya Wilaya ya
Mtwara kama Afisa Ushirika daraja la tatu. Mwaka 1990 alienda masomoni kwa
ajili ya masomo ya Diploma ya Juu ya Usimamizi wa masuala ya Ushirika kwenye
chuo cha Ushirika Moshi na kuhitimu mwaka 1991.
Mwaka
1992 hadi
1993 Marehemu Francis Eprem Luambano alipata elimu ya Stashahada ya
Uzamili kwenye Chuo cha Usimamizi wa Fedha ‘IFM’. Marehemu Francis Eprem
Luambano alihitimu Shahada ya Uzamili ya
Utawala wa Biashara kwenye chuo cha Biashara cha India (Indian Institute
of Foreign Trade) mwaka 2012
Marehemu
Francis Eprem Luambano alihamia Manispaa ya Ilala mwaka Desemba, 2003 hadi
kufariki kwake ameitumikia Manispaa ya Ilala kwa kipindi cha miaka 13 na katika
kipindi chote hicho Marehemu alikuwa ni mchapakazi aliyekuwa na ubunifu. Aliyeipenda
kazi yake na kuifanya kwa weledi mkubwa uliowezesha kuwepo kwa mafanikio katika
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala. Katika Manispaa ya Ilala amewezesha kuboresha
ukusanyaji wa mapato hususan kodi ya Majengo, leseni za biashara na kodi za
mabango kwa kuratibu zoezi la ukusanyaji takwimu za walipa kodi (BRN-Mapato). Marehemu aliwaheshimu Viongozi wake na watumishi
wenzake. Aidha alikuwa tayari kukoselewa pale ilipoonekana kuna dosari katika
kutekeleza wajibu wake. Tabia yake ya kumjali kila mtu ilimfanya kuwa kimbilio
la wenye kuhitaji msaada wa hali na mali kutoka kwake. Alipenda utani na
kuamini kuwa mafanikio yoyote yatatokana na kufanya kazi kwa pamoja jambo
ambalo alifanikiwa kulitekeleza katika Idara aliyokuwa akiiongoza. Hakika Manispaa ya Ilala imepoteza mtumishi
ambaye bado mchango wake ulikuwa unahitajika katika kuwaletea maendeleo Wananchi wa Ilala.
Mungu ailaze mahali pema peponi
roho ya marehemu ndugu yetu, mpendwa wetu FRANCIS
EPREM LUAMBANO