MANISPAA YA ILALA YAWAPONGEZA WALIMU NA VIONGOZI WALIOFANYA VIZURI MWAKA 2018

Na: Hashim Jumbe
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, kupitia Idara yake ya Elimu Msingi, imetoa tuzo kwa Walimu na Viongozi wa Shule za Msingi zilizofanya vizuri katika Matokeo ya Mtihani wa kumaliza Elimu Msingi na Upimaji wa Kitaifa Darasa la Nne kwa mwaka 2018.

Tuzo hizo zilizotolewa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala siku ya jana, zilikuwa na lengo la kuwatambua na kuwapongeza Walimu na Viongozi wote waliofanikisha upatikanaji wa matokeo mazuri kwa mwaka uliopita.

Akitoa taarifa ya tathmini ya Idara ya Elimu Msingi kwa mwaka 2018, Afisa Elimu Msingi Manispaa ya Ilala, Bi. Elizabeth Thomas alisema "Katika Matokeo ya Mtihani wa kumaliza Elimu Msingi mwaka 2018, Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ilishika nafasi ya Nne (4) Kitaifa na ilishika nafasi ya Pili (2) Kimkoa, huku ikiwa na wastani wa ufaulu wa 95.59% ikiwa ni ongezeko la 3.13% ukilinganisha na matokeo ya mwaka 2017 ambapo tulipata wastani wa 92.46%"

Aidha, Bi. Elizabeth Thomas alitoa na taarifa ya Matokeo ya Upimaji wa Kitaifa Darasa la Nne kwa mwaka 2018, ambapo alisema "Katika Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne kwa mwaka 2018, Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, imeshika nafasi ya Nne (4) Kitaifa na nafasi ya Kwanza (1) Kimkoa, tukiwa na wastani wa ufaulu wa 99.56% ikiwa ni ongezeko la 0.59% ukilinganisha na matokeo ya mwaka 2017 tuliyopata wastani wa 98.97%".

Katika eneo la Michezo, Afisa Elimu Msingi alitoa taarifa ya timu ya Wilaya ya Ilala, imeweza kuibuka mshindi wa jumla kwa miaka mitatu mfululizo katika mashindano ya UMITASHUMTA kwa ngazi ya Mkoa "kuna Walimu waliweza kuwaandaa vizuri Wanamichezo wetu, tuliweza kuweka kambi ambayo ilitusaidia kuwaandaa Watoto vizuri, hivyo ikatusaidia kufanya vizuri kwa miaka mitatu mfululizo" alisema Bi. Elizabeth Thomas

Kwa mafanikio hayo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Bw. Jumanne Shauri aliweza kutoa tuzo katika vipengele vifuatavyo;

  1. Kipengele cha Mazingira
  2. Kipengele cha Uongozi
  3. Kipengele cha Hamasa
  4. Kipengele cha Sanaa na Uongozi
  5. Kipengele cha Ubunifu
  6. Kipengele cha usimamizi wa ujenzi
  7. Kipengele cha Ufaulu wa Mtihani wa Darasa la Saba na Upimaji wa Kitaifa Darasa la Nne
  8. Kipengele cha Utendaji wa Heshima



Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi