Historia itamkumbuka Rais Magufuli ‘Wananchi Ilala kunufaika na miradi ya Kimkakati na Hospitali ya Wilaya’

Na: Hashim Jumbe

NELSON Mandela, mzaliwa wa Kijiji cha Mzevo, nchini Afrika Kusini mwaka 1918, Kiongozi wa mapambano dhidi ya siasa ya ubaguzi wa rangi, mfungwa jela kwa miaka 27, alafu Rais wa Kwanza aliyechaguliwa Kidemokrasia katika nchi yake na Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel ya mwaka 1993 aliwahi kusema “it always seems impossible until it’s done” kwa tafsiri isiyo rasmi sana alimaanisha “mara zote huonekana haliwezekani mpaka lifanikiwe”

Kauli hii inadhihirisha wazi kuwa maendeleo si jambo rahisi, kwa maana wapo watakaobeza na wapo watakaopongeza, kama ilivyoonekana katika siku za mwanzo za utawala wa Rais Magufuli, kuna ambao hawakuamini kuwa hii ni safari ya kuelekea ‘Kaanan’ mpaka macho yao yaliposhuhudia mambo mbalimbali ya kimaendeleo yakitekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano, labda ni hulka ya Wanadamu ambao mpaka waone ndiyo waamini kama wasemavyo Waingereza “seeing is believing” wakiwa na maana kuwa “kuona ni kuamini”

Sasa ni ukweli usiopingika kuwa Rais Magufuli ametufikisha pale ambapo pengine tusingeweza kufika au tungechelewa kufika, kwa kipindi cha miaka minne tu jina lake limejiandika kwenye vitabu vya historia ya nchi yetu, atakumbukwa vizazi na vizazi kwa mafanikio makubwa aliyoyafanya katika huduma za kijamii na nyenginezo.

Pamoja na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimaendeleo kama vile ujenzi wa reli ya kisasa ‘SGR’, mradi wa kufua umeme katika mto Rufiji na miradi mingineyo, lakini pia Serikali imeanzisha miradi ya mbalimbali ya kimaendeleo katika Halmashauri zote nchini, lengo likiwa ni kuboresha huduma, kuziongezea uwezo wa kukusanya mapato na kupunguza utegemezi wa kibajeti kutoka Serikali Kuu. Manispaa ya Ilala ni moja kati ya Halmashauri zinazonufaika na miradi mikubwa inayofadhiliwa na Serikali Kuu, miradi hiyo ni kama vile;

Ø  Ujenzi wa Machinjio ya Kisasa ya Vingunguti

Mradi wa Ujenzi wa Machinjio ya kisasa ya Vingunguti ni moja kati ya Miradi miwili ya Kimkakati inayotekelezwa na Manispaa ya Ilala kupitia Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ambapo miradi hii inalenga kuziwezesha Halmashauri kujitegemea kimapato ilikutoa huduma bora zaidi na zenye uhakika kwa Wananchi.

“Uamuzi wa Serikali kujenga machinjio haya, utaifanya nyama inayotoka hapa ikubalike kwenye masoko ya nje ya nchi, hatua mbayo itaongeza mzunguko wa fedha kwenye eneo hili wakati Serikali na Manispaa watanufaika kwani kutakuwa naongezeko la makusanyo ya kodi” alisema Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa alipofanya ziara ya kufuatilia ujenzi wa machinjio ya Vingunguti, tarehe 3 Desemba, 2019

Ujenzi wa Machinjio ya kisasa ya Vingunguti, unatekelezwa na Mkandarasi ambaye ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na ujenzi huo ulianza rasmi tarehe 08 Julai 2019, ambapo gharama za utekelezaji wa mradi ni TSh. 12.4 Bilioni, ambapo TSh. 8.5 Bilioni ni fedha kutoka Serikali Kuu na TSh. 3.9 Bilioni ni fedha za makusanyo ya ndani ya Halmashauri na mpaka tarehe 19 Me, 2020 ujenzi ulikuwa umefikia 85%

 

 

Aidha, ujenzi wa Machinjio ya Vingunguti umefuatia mazingira duni ya Wafanyabiashara ya mifugo na mazao yake pamoja na uuzwaji wa nyama katika mazingira yasiyo salama kwa afya ya mlaji, hivyo Serikali imeamua kuboresha huduma za uchinjaji wa mifugo na kuongeza idadi ya mifugo inayochinjwa kila siku kutoka wastani wa mifugo 500 hadi mifugo1,500  kwa siku na pia kuboresha usafi wa nyama inayopatikana kwenye machinjio hayo.



Ujenzi wa Machinjio ya Kisasa ya Vingunguti, ukiwa umefikia 85% hadi tarehe 18 Mei, 

2020


 

Ø  Ujenzi wa Soko la Kisutu

Miaka 56 imepita tangu Soko la Kisutu lianzishwe, Soko hilo ambalo mpaka kufikia mwaka 2018 lilikuwa na Wafanyabiashara wapatao 633, ambao ni wauza kuku hai na wakuchinja 201 na kundi la pili ni la Wafanyabiashara 432 ambao ni Mama na Babalishe, wauza nafaka, matunda na mbogamboga.

 Aidha, ujenzi wa Soko la kisasa la Kisutu ulioanza rasmi tarehe 12 Disemba, 2018 chini ya Mkandarasi ‘Mohammedi Builders Ltd’ unatarajia kukamilika mwezi Julai, 2020

Kukamilika kwa Soko hilo la kisasa lenye ghorofa Nne (4) litaweza kuchukua Wafanyabiashara 1,500 na litakuwa na huduma mbalimbali muhimu kama vile Benki, Mabucha, Machinjioya Kuku, Maegesho ya magari na eneo la biashara.

Gharama za mradi wa ujenzi Soko la Kisutu ni Shilingi13.4 Bilioni ambapo Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imetoa Shilingi 12.1 Bilioni kwaajili ya kutekeleza Mradi huo wa Kimkakati na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imechangia Shilingi 1.3 Bilioni, lengo la Mradi ni kuhakikisha Halmashauri inaongeza mapato ya ndani na kupunguza utegemezi wa kibajeti kutoka Serikali Kuu.


Muonekano wa Ujenzi wa Soko la Kisutu


Ø  Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya Kivule

Historia mpya imeandikwa kwenye Sekta ya Afya tangu kupatikana kwa Uhuru wa Nchi yetu mwaka 1961, kwani Hospitali mpya za Wilaya 70 zimejengwa katika awamu hii ya 5 inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli na kufanya nchi yetu hadi sasa kuwa na Hospitali za Wilaya 147

“Tangu tupate uhuru tulikuwa na hospitali za wilaya 77 lakini sasa Serikali ya Awamu ya Tano inaenda kuweka historia kwa mageuzi makubwa yanayofanyika katika sekta hii ya afya na tumejipanga kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata huduma bora za afya” hayo yalikuwa ni maneno ya msisitizo kutoka kwa Mhe. Seleman Jafo ambaye ni Waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI mwaka 2018 alipokuwa akizungumzakatika kipindi cha Tunatekelezakilichorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Kati ya Hospitali hizo 70 za Wilaya zilizojengwa, moja wapo ni Hospitali ya Wilaya ya Ilala iliyopo Kivule, ujenzi wa Hospitali hii ni mkakati wa Serikali na jitihada zake katika kuboresha huduma za afya kwa Wananchi wake na kupunguza adha katika kupata huduma za afya.




Muonekano wa moja kati ya Majengo 7 yaliyojengwa kwenye Hospitali ya Wilaya ya Kivule



Aidha, ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Kivule umekuja kufuatia iliyokuwa hospitali ya Wilaya ya Amana kupandishwa hadhi na kuwa Hospitali ya Mkoa, hivyo Wilaya ya Ilala kukosa Hospitali ya Wilaya, jambo linalowalazimu Wananchi wa Wilaya hii hususani wanaoishi maeneo ya pembezoni mwa mji kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya katika Hospitali ya Mnazi Mmoja.

Kutokana na adha hiyo kwa wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya haswa waakina Mama wajawazito ambao wengi wao wanakuwa kwenye hatari ya kupoteza maisha kutokana na kuchelewa kupata huduma stahiki, hivyo Serikali ya awamu ya Tano kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ikaamua kujenga Hospitali ya Wilaya iliyopo Kivule.

Ujenzi wa Hospitali ya Kivule umelenga kuongeza nafasi kwa ajili ya wagonjwa kupata huduma za afya kwa urahisi, lakini pia ni kutekeleza Sera ya Taifa inayosisitiza kila Wilaya kuwa na Hospitali yenye hadhi ya Wilaya.

Sambamba na hilo, lakini pia Hospitali hii itakuwa na madaktari bingwa na wataalamu wenye uweledi wa kutosha, na hii itasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya Amana, hivyo kusogeza huduma za afya karibu na wananchi

Ujenzi wa Hospitalii hii utahudumia Wananchi kutoka kwenye Kata za Kivule, Msongola, Kitunda, Kipunguni, Majohe, Mzinga na Wananchi wa Kata nyengine za jirani nao watanufaika na matibabu Hospitalini hapo ikiwemo huduma za kibingwa na rufaa kutoka kwenye Zahanati na Vituo vya Afya.

Gharama za ujenzi wa Hospitali ya Kivule ni Shilingi Bilioni 1.5, fedha kutoka Serikali Kuu na unajumuisha majengo Saba (7) ambayo ni; jengo la Utawala, jengo la Wazazi, jengo la Mionzi, jengo la Ufuaji, jengo la Stoo ya Dawa na jengo la Maabara, lakini sambamba na majengo hayo, Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imeanza ujenzi wa jengo la huduma za haraka ‘fast track’linalojengwa kwa fedha za ndani



Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Seleman Jafo (wa pili kulia) akimsikiliza Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Ndugu Jumanne Shauri, alipotembelea ujenzi wa jengo la huduma za haraka ‘fast track’ Hospitali ya Wilaya ya Kivule



Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi