Na;
Hucky Hamis na Shamimu Msuya
Halmashauri
ya Manispaa ya Ilala imewakutanisha walimu wote wa shule za msingi katika Manispaa hiyo siku ya Jumanne 29. 09. 2020 kwenye Kikao Kazi cha awamu ya tatu
kilichofanyika kwenye ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere, Posta
jijini Dar es Salaam ili kujadili mafanikio na kutatua changamoto za walimu
hao.
Baadhi ya Walimu waliofika kwenye Kikao Kazi
Kadhalika,
Afisa Elimu wa Manispaa ya Ilala Bi. Elizabeth Thomas ametanguliza shukrani na
pongezi za dhati kwa walimu hao kwa majukumu wanayofanya katika kufundisha na
kuhudumia wanafunzi wa aina zote jambo ambalo limeifanya Manispaa hiyo kuwa
kwenye nafasi za juu kitaaluma na kueleza kuwa tangu mwaka 2015 kumekuwa na
ongezeko kubwa la idadi ya uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza,
kuimarika kwa miundombinu ya shule ikiwemo nyumba za walimu na upatikanaji wa
maji na ongezeko la samani za shule ambazo zimetolewa na Benki ya CRDB ambao ni
wadau wa elimu.
Aidha,
Walimu walipewa nafasi ya kuuliza maswali na kutoa changamoto wanazopitia
ambapo Mwalimu Henry alizungumza juu ya changamoto wanazopitia kwenye ulipwaji
wa posho za likizo.
Akijibu
changamoto hiyo, Afisa Utumishi wa Manispaa ya Ilala Bwana Said Ismail amesema “Kwanza niwatoe wasiwasi walimu wangu
kwasababu hiyo changamoto ipo kwenye hatua za ufumbuzi na linashughulikiwa na
TAMISEMI kwa kuwa imekuwa ni changamoto kubwa na siyo changamoto yenu walimu
pekee bali ni kwa watumishi wote, kwahiyo tuwe wavumilivu wakati jambo hili
linashughulikiwa”
Afisa Utumishi wa Manispaa ya Ilala Bw. Said Ismail akijibu changamoto za kiutumishi
Sambamba
na hayo, suala la upashanaji habari kati ya wananchi na serikali halikuachwa
nyuma ambapo Afisa Uhusiano wa Manispaa ya Ilala kutoka kitengo cha Habari,
Uhusiano na Mawasiliano Bi Tabu Shaibu amesema “Napenda kuwakaribisha walimu
wetu wa elimu msingi kufanya kazi na sisi kwani sisi ni daraja kati ya vyombo
vya habari na wananchi, lakini idara ya Elimu Msingi inajitahidi na kunifanya nionekane nafanya kazi sana”
aliendelea kwa kuwakaribisha sana walimu kushirikiana na idara ya habari ya
Manispaa katika kutatua changamoto za ndani badala ya kutumia vyombo vya nje
ili kusaidia kupata ufumbuzi kwa haraka zaidi.
Pia,
Afisa Elimu Msingi wa Manispaa Bi. Elizabeth Thomas alimalizia mjadala kwa
kuwakumbusha walimu kujiandaa kustaafu ili kuepusha changamoto wanazokutana
nazo baada ya kustaafu wakiwa hawajajiandaa ikiwemo kuandika miaka sahihi na
kujipanga kimaisha na mwisho kumkaribisha Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Bwana
Jumanne Shauri kufunga kikao hicho na alifunga kwa kuwatia moyo walimu kuwa
wajivunie kuwa na taaluma hiyo kwani ni miongoni mwa taaluma ambazo hazina
mwisho wa kufanya kazi.
Kikao
kazi hicho cha Manispaa ya Ilala Idara ya Elimu Msingi hufanyika mara moja kila
mwaka na mwaka huu 2020 kimefanyika tarehe 22, 28 na 29 Septemba kikihusisha
jumla ya walimu 3,700 wa Manispaa ya Ilala na kufayika kwa awamu tatu.