“SERIKALI INATHAMINI NA KUHESHIMU MCHANGO WA WAZEE NCHINI” - MH LUDIGIJA

 

Na Jafari & Rayyah Kimwaga

 Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mh Ng’wilabuzu Ludigija amesema Serekali inatambua na kuthamini mchango wa wazee katika maendeleo ya nchi.

Ameyasema hayo kwenye maadhimisho ya siku ya wazee yaliyofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam Jumamosi tarehe 3 mwezi huu alipokua anamuwakilisha Mkuu wa Mkoa

Mh Ludigija amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa wazee kwani tangu enzi za kutafuta uhuru wazee walitumika sana katika jitihada hizo na kuzaa matunda makubwa.

 

 

                   Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mh. Ng’wilabuzu Ludigija akihotubia

 

Aidha, Mh Ludigija amesisitiza kuwa katika kuthamini mchango wa wazee mkoa wa Dar es Salaam umeunda mabaraza 506 ya Wazee kwa ngazi zote  kuanzia Kata mpaka ngazi ya Mkoa ambayo yatasaidia kushughulikia changamoto za wazee.

“Na mimi nitoe wito tu mabaraza haya yahakikishe yanafanya kazi. Maafisa Ustawi, Waganga Wakuu na Wakurugenzi muhakikishe mnayawezesha mabaraza haya yaweze kufanya kazi kama ambavyo Serikali imekusudia.”  Aliongeza

 

 

Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mh. Ng’wilabuzu Ludigija akimkabidhi muongozo wa Mabaraza    Mwenyekiti Baraza la Wazee mkoa wa Dar es Salaam Mzee Matimbwa

 

Pia Mkuu wa Wilaya Mh Ludigija amesema kuanzia mwezi wa nne mkoa wa Dar es Salaam umetumia zaidi ya milioni 800  kugharamia matibabu ya makundi maalum ikiwemo wazee.

Sanjari na hayo aliongeza kuwa mzee hapaswi kukaa nyuma ili kupata huduma yoyote ikiwemo matibabu na katika ofisi zote za umma na katika kulihakikisha hilo Serikali imeweka Maafisa Ustawi katika kila kituo cha afya watakao saidia mzee kupata huduma kwa haraka na kwa ufanisi mkubwa.

“Katika mkoa wa Dar es Salaam kuna vituo takribani 122 ambavyo tayari maafisa utawi wapo kwahiyo wazee wazitumie ofisi hizo za ustawi ili wapate matibabu kwa wakati”

 

 

Picha ya pamoja ya Mkuu wa Wilaya na Wenyeviti wa mabaraza ya wazee Mkoa wa Dar es Salaam

 

Pamoja na hayo, Serikali imetoa vitambulisho vya wazee vitakavyomuwezesha mzee kupata msamaha wa matibabu na kupata matibabu bure katika vituo vya afya vya Serikali kwa sasa na baadae vituo vya binafsi pia.

 Naye Mwenyekiti Baraza la Wazee mkoa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Ilala Mzee Matimbwa akizungumzia changamoto za wazee alisema wazee wengi wanapoteza maisha kwa kukosekana kwa taratibu bora za kuwatunza wazee.

 

 

                                Mkuu wa Wilaya akikabidhi fimbo nyeupe

 

 “Tangu 2003 bado sera ya wazee inaendelea kuwaongoza na mpaka sasa bado haijawa sheria. Sisi tunataka sera hiyo iwe sheria ili haki za wazee ziweze kuthaminiwa na kulindwa lakini muda unaenda. Watambuliwe wazee na haki zao na isiwe kwa hisani tu”

Kwa kujibu swala hilo kaimu mkuu wa mkoa amesema Serikali ipo katika mchakato wa kuhakikisha sheria ya inaundwa na kupitishwa ili kusaidia haki za wazee kulindwa na kuthaminiwa.

 

 

           Baadhi ya Wazee walisubiri kupata huduma ambazo zilikua zikitolewa bila malipo

 

 Kidunia siku ya Wazee huadhimishwa tarehe 1 Mwezi wa kumi kila mwaka na maadhimisho hayo kwa Mkoa wa Dar es Salaam yalikua na kauli mbiu ya “Familia na jamii tuwajibike kuwatunza wazee”

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi