Wanafunzi Ilala waahidi kufanya vizuri mtihani wa kumaliza Darasa la Saba mwaka 2020

 Na: Hashim Jumbe

Wanafunzi wa Darasa la Saba katika Shule za Manispaa ya Ilala, leo wametoa ahadi ya kufanya vizuri katika mtihani wao wa kumaliza elimu ya msingi unaotarajiwa kufanyika nchini kote tarehe 07-08 Oktoba, 2020.

 Ahadi hiyo ya kufanya vizuri katika mtihani wao wameitoa mbele ya Afisa Elimu Msingi Manispaa ya Ilala Bi. Elizabeth Thomas alipotembelea Shule ya Msingi Buguruni na Majani ya Chai na kuzungumza na Watahiniwa hao kwa niaba ya wenzao wote watakaofanya mtihani huo.

 Wanafunzi hao walitoa ahadi ya kufanya vizuri kwa kuzingatia maandalizi waliyoyafanya na matokeo ya mtihani wa utimilifu kwa ngazi ya Wilaya na Mkoa yalizidi kuwapa ujasiri huku wakitumia mitihani hiyo kujiandaa vizuri zaidi.

"Tumefanya maandalizi ya kutosha na tunaimani tutafanya vizuri zaidi na wote tutafaulu kwenda Sekondari" alisema mmoja kati ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Majani ya Chai

Akizungumza na Wanafunzi hao, Afisa Elimu Msingi Manispaa ya Ilala Bi. Elizabeth Thomas aliwataka wanafunzi hao kuanza kwa kumtanguliza Mungu na kujiamini huku wakizingatia maelekezo yote ya mtihani "ninawatakia heri wanafunzi wote, mfanye vizuri na mie nitakuwa wa kwanza kuangalia matokeo ya shule yenu, sasa msije mkawaangusha walimu wenu"

Mtihani wa kumaliza elimu ya msingi (PSLE) 2020 kwa Manispaa ya Ilala utahusisha Jumla ya Watahiniwa 28,280 ambapo Wavulana ni 13,802 na Wasichana 14,478









 

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi