Katibu Tawala Wilaya ya Ilala aongoza zoezi la usafi wa mwisho wa mwezi

Katika kuendeleza kampeni ya Safisha, Pendezesha Dar es Salaam iliyoanzishwa mwaka mmoja uliopita na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Amos Makalla, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kushirikiana na wadau mbalimbali mazingira, Leo tarehe 28 Januari, 2023 imefanya usafi katika maeneo yanayozunguka masoko ya Karume na Machinga Complex.


Zoezi hilo lililoongozwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala Bi. Charangwa Makwiro alieambatana na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Eng. Amani Mafuru pamoja na Wakuu wa Idara limefanyika ikiwa ni muendelezo wa utaratibu uliowekwa wa kufanya usafi jumuishi kila ifikapo Jumamosi ya mwisho wa mwezi.


Akiongea na wadau hao wa mazingira pamoja na wananchi walioshiriki katika zoezi hilo Eng. Mafuru amewashukuru wote waliojitokeza katika zoezi hilo na kuwaomba usafi usifanyike mwisho wa mwezi tu bali liwe ni zoezi endelevu kwani ndio ajenda kuu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.


"Usafi ni ajenda kuu ya Mhe.Rais hivyo yatupasa sote tulitekeleze wazo hilo kwa kusafisha mazingira yetu mara kwa mara." Amesema

Kampeni ya Safisha, Pendezesha Dar es Salaam imekuwa na mwitikio chanya kwa wananchi na kuzaa matunda kwa kulifanya Jiji la Dar es Salaam kuwa miongoni mwa Majiji masafi Barani Afrika kwa kushika nafasi ya sita.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi