Suala la usomaji shuleni linahitaji wanafunzi kuwa na afya bora na utimamu wa akili, hivyo wanafunzi wakipata chakula shuleni itawasaidia kujenga afya bora na hivyo kumudu kuelewa yale wanayojifunza shuleni na kufanya matokeo yao na ufaulu kwa ujumla kuwa wa juu.
Mnamo tarehe 29 Octoba, 2021 Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Teknolojia ilizindua muongozo wa kitaifa wa utoaji wa huduma za chakula na lishe kwa wanafunzi mashuleni wenye lengo la kuwaelekeza wadau wa elimu nchini kote namna bora ya kutekeleza utoaji wa huduma ya chakula na lishe mashuleni.
Katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Muongozo huo umepokelewa kwa muitikio chanya kwani shule nyingi zimeanza kutoa huduma ya chakula mchana na kuwawezesha wanafunzi kuzingatia masomo yao kikamilifu. Shule ya Sekondari Jamhuri ni moja ya shule ambazo zimeanza kutoa huduma ya chakula kwa wanafunzi wake. Na kutokana na maelezo ya Mkuu wa shule hiyo Mwl. Boniphase Mwalwego amesema kuwa kuanzishwa kwa huduma ya chakula katika shule yake kumesaidia sana hali ya ufaulu kuwa juu hasa kwa wanafunzi wa kidato cha pili na kidato cha nne waliofanya mitihani yao ya Taifa mwaka jana wa 2022.
“Asilimia 75 ya wanafunzi wa kidato cha pili katika shule yetu wamepata ufaulu wa daraja la kwanza, na katika wanafunzi wote waliofanya mtihani huo hakuna aliyerudia kidato. Kwa upande wa Kidato cha nne asilimia 80 ya wanafunzi waliofanya mtihani huo wamepata daraja la kwanza.” Amesema Mwl. Mwalwego
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Jamhuri wakipata chakula |
Aidha amesema kuwa huduma ya chakula na lishe mashuleni inasaidia kujenga akili za wanafunzi kikamilifu. Kwa sababu hivi sasa wanafunzi wanaojiandaa na mitihani wanaanza masomo yao saa 1 asubuhi, hivyo sio rahisi kwa wao kupata chakula nyumbani kabla ya kwenda shule. Kupata chakula shuleni kunawasaidia wanafunzi kuwa wasikivu na kuzingatia kile wanachofundishwa wawapo darasani na mazingira ya shule kwa ujumla.
Vilevile utoaji wa chakula umepunguza kasi ya utoro kwa wanafunzi na kuwapa motisha ya kusoma. Hapo awali wanafunzi walikuwa na tabia ya kutoroka kabla ya vipindi kuisha kutokana na njaa, lakini kufuatia kuanzishwa kwa huduma ya chakula katika shule yao, wanafunzi wamekuwa wakihudhuria vipindi vyote darasani na kuachana na tabia ya utoro.
Mwl. Mwalwego pia amesema kuwa kwa miaka inayoendelea ana Imani kuwa uanzishwaji wa utoaji wa huduma ya chakula na lishe mashuleni utaongeza hali ya ufaulu zaidi kwa wanafunzi wao kwani akili zao zinajengeka kwa kupata lishe kwa wakati katika muda wote wawapo katika mazingira ya shule.
Sambamba na hilo wanafunzi wa shule hiyo wametoa shukrani zao za dhati kwa Serikali kwa kuanzisha muongozo huu wa chakula na lishe mashuleni, kwani umekuwa ni chachu kubwa na umesaidia kuleta hamasa kwa wanafunzi katika mchakato mzima wa kusoma na kujifunza.
Ikumbukwe kuwa moja ya vitu ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amevipa kipaumbele ni suala la Lishe bora nchini. Na hii ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha nchi inaondokana na tatizo la utapiamlo na wananchi wake wanakuwa na afya bora na kuwawezesha kufanya kazi kwa bidi kwa maslahi mapana ya mwananchi mmoja mmoja na Taifa zima kwa ujumla.