Na,Judith Damas,Mariam Hassan na Exsebia.
Mkuu wa Wilaya Ya Ilala Mh.Ng’wilabuzu Ludigija ametoa maagizo kwa wafanyabiashara wote wa masoko ya Bombom, Minazi Mirefu na Kigilagila ifikiapo tarehe 8 Februari 2021 wawe wameahamia kwenye masoko hayo mapya na pia atagawa vizimba kwa kila mmoja wao.
Amesema hayo katika ziara yake ya kukagua ukamilikaji wa ujenzi wa masoko hayo akiambatana na Katibu tawala wa Wilaya ya Ilala na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala na Mkuu wa Masoko Manispaa ya Ilala leo tarehe 27 Januari 2021.
“Ninawaomba muwe wavumilivu zoezi litafanyika
kwa siku tano hadi kufikia tarehe 8 February 2021 nitawagawia vizimba kulingana
na Orodha ya wafanyabiashara kupitia jina kwa jina na kila mmoja awe na
kitambulisho cha Mpiga kura au Taifa.”
Mkuu wa Wilaya ya Ilala akiongea na wafanya biashara wa soko la BOMBOM
Pia, Mkuu wa Wilaya ameipongeza
Serikali kwa miundombinu mizuri ambayo itawasaidia wafanyabiashara kusafirisha mizigo yao
kiurahisi.
“Naipongeza Serikali ya awamu ya tano kwa
miundombinu mizuri hivyo nawasihi mlinde miundombinu na kutunza mazingira ili
kuepuka magonjwa ya milipuko”
Hata hivyo, Mh. Ludigija amewaasa
wafanyabiashara waache tabia ya kupangisha fremu na atakayebainika atachukuliwa
hatua za kisheria.
Mwenyekiti wa Soko la Bombom Bw.
Muhidini Waziri ameishukuru Serikali
pamoja na Manispaa ya Ilala kwa kuwajengea soko la kisasa kwani awali
soko hilo lilikuwa linajaa maji kipindi cha mvua hivyo biashara inakuwa ngumu
na kina mama walikuwa wanapata tabu kuingia sokoni.
Vilevile Mkurugenzi wa Manispaa ya
Ilala Ndug. Jumanne Shauri amesema kujengwa kwa masoko hayo inapunguza adha kwa
wananchi kusafiri sehemu za mbali kwenda kuchukua bidhaa.
Aidha, Mkurugenzi wa Manispaa ya
Ilala alisema kutokana na kodi inayopatikana katika masoko hayo inasaidia uwepo
wa huduma nyingine za kijamii.
“Sisi kama Manispaa ya Ilala tuna
takribani masoko 36 hivyo kutokana na kodi inayotolewa inasaidia kujenga
madarasa na vituo vya afya”