Na.Rosetha Gange na Judith Damas
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Amos Makala leo Mei, 31 2021 amefanya
kikao kazi na Madiwani,
wakuu wa idara, pamoja na watendaji kata katika ukumbi
wa Arnatoglou uliopo Mnazi Mmoja Jijini
Dar es Salaam lengo kubwa likiwa ni
kufahamiana na kuwaelekeza vipaumbele vyake akiwa ni Mkuu mpya
wa Mkoa wa Dar es Salaam ikiwemo usafi,utekelezaji wa ilani ya Chama, kutatua
kero za wananchi,utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo,kuwapanga
wamachinga pamoja na ulinzi na usalama.
Aidha, Mhe. Makala amesisitiza suala la usafi katika Halmashauri ya jiji
la Dar es Salaam kwani hali ya usafi katika Jiji hili hairidhishi hivyo amewataka watumishi pamoja na watendaji
wa Kata kupanga mikakati ya haraka ili kulirejesha Jiji katika mandhari ya
usafi kwani ndio kitovu cha wageni katika nchi yetu ya Tanzania.
“Jiji la Dar es salaam ni Jiji kubwa,watu mbalimbali
wanafika hapa,Kwa hali ilivyo sasa hali si nzuri.Sijaridhishwa na hali ya usafi
katika jiji la Dar es Salaam kwani hapa ndio uso wa Tanzania.Lazima jitihada za
haraka zifanyike.”
Katika kuhakikisha suala hili linatekelezeka Mh.Makala amekusudia
kuzindua kampeni ya usafi katika jiji la Dar es salaam na kuwasisitizia
watendaji wote wa jiji wakawe wasimamizi wa zoezi hili na kuwa usafi uanze
kwenye kaya,mitaa, kata na katika Halmashauri ya jiji lao.
Sambamba na hilo Mhe. Makala amesema kuwa atakuja na mpango wa kuwapanga
upya wamachinga na wafanyabiashara ndogo
ndogo katika jiji la Dar es salaam ili jiji liwe kwenye muonekano mzuri na liwe
katika hali ya usafi. Pia amesisitiza kuwa kutokuwa na usimamizi na ufuatiliaji
madhubuti kunafanya jiji kuonekana katika hali ya uchafu na wahalifu hutumia vibanda hivyo kama
maficho yao wakati wa usiku.
Akitoa shukrani kwa niaba ya watendaji wote wa Jiji la Dar es Salaam
Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Mh.Omary Kumbilamoto alimpongeza Mh.Makala kwa hotuba nzuri na
kuahidi kuyatekeleza yale yote aliyowaagiza na kumuhakikishia ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza
majukumu yake.