Na: Hashim Jumbe
Watumishi wa Idara ya Elimu Msingi, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, chini ya Umoja wa Viongozi wa Elimu Jiji la Dar es Salaam (UVEMI) jana tarehe 21 Mei, 2021 wamefanya hafla fupi ya kumuaga aliyekuwa Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri hiyo ambayo zamani ilikuwa ikiitwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala
Hafla hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa Masia uliopo Segerea, ilihudhuriwa na watu mbalimbali akiwemo Afisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Ndugu Abdul Maulid ambaye alikuwa Mgeni rasmi, Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Mhe. Omary Kumbilamoto, baadhi ya Wakuu wa Idara za Halmashauri waliojumuika kwenye hafla hiyo wakiongozwa na Afisa Utumishi Mkuu, Bi. Benadetha Mwaikambo, Wathibiti Ubora wa Shule, Katibu Msaidizi TSC Wilaya ya Ilala, Walimu Wakuu kutoka Shule za Serikali na Shule Binafsi, Maafisa Elimu Kata pamoja na Maafisa wa Idara ya Elimu Msingi waliopo Ofisi ya Idara ya Elimu Msingi Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wakiongozwa na Bi. Sipora Tenga ambaye ni Afisa Elimu Msingi.
Bi. Elizabeth Thomas amestaafu kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma akiwa ameihudumia Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kwa mafanikio makubwa tangu alipopata cheo cha Afisa Elimu Msingi kuanzia Mei, 2012 hadi Disemba 2020 alipostaafu.
"Mama Thomas alikuwa zaidi ya cheo chake alijipambanua kama Kiongozi, Mlezi, Mshauri na alikuwa Mama wa wote, hakutubagua, wote alituona tupo sawa na kututhamini katika usawa, alitufundisha kazi, na alitamani kuona kila Mtu anafanya kazi kwa moyo na furaha" Mwl. Simon Mndendemi wakati akisoma risala kwa mgeni rasmi
Akizungumza katika hafla hiyo, Afisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Ndugu Abdul Maulid, ambaye alikuwa Mgeni rasmi aliwaasa Watumishi waliopo kuendelea kufanya kazi kwa kujituma na kumpa ushirikiano Afisa Elimu mpya "Watumishi mliopo hapa, nyie ni kiungo muhimu katika kumsaidia Mkuu wenu mpya wa Idara kutekeleza majukumu yake, ni matumaini yangu kuwa mtampa ushirikiano wa kutosha kama mlivyokuwa mkimpa Mama Thomas"
Naye Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Mhe. Omary Kumbilamoto alimpa sifa Mama Thomas kwa utendaji wake wa kazi aliokuwa nao "Siku zote nimekuwa nikimsifu Mama Thomas kwa jinsi alivyokuwa akikimbizana kutekeleza miradi yote ya idara yake kama ujenzi wa vyumba vya Madarasa, Ofisi za Walimu, matundu ya vyoo na mengineyo, utendaji wake na kujituma iliturahisishia hata sisi Madiwani, na ilifikia hatua alikuwa akileta taarifa kwenye vikao tunasema tu ipite"
Naye Bi. Sipora Tenga, ambaye ni Afisa Elimu Msingi Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam akimuelezea alivyomfaham Bi. Elizabeth Thomas alisema "Bi. Elizabeth Thomas alikuwa ni mshauri mzuri, alikuwa zaidi ya Mama, na alipenda Watumishi wajiendeleze kielimu na ndiye aliyenifanya niende masomoni kujiendeleza kielimu, wakati huo nikiwa Mwalimu nafundisha Shule ya Msingi Olympio"
Aidha, Mama Thomas amestaafu huku akiacha sifa na heshima kwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambayo ilikuwa Manispaa ya Ilala, utendaji wake umeifanya Halmashauri hii kufanya vizuri kwenye Taaluma na Michezo, kwani ameisadia Halmashauri kuingia kwenye '10 bora' matokeo ya Kitaifa ya Darasa la Saba na Upimaji wa Darasa la Nne, hakika Jiji la Dar es Salaam wataendelea kumkumbuka kwa mchango wake.
Katika Hafla hiyo Walimu Wakuu wa Shule za Serikali walimpatia mstaafu huyo zawadi ya Gari aina ya 'X-Trail New Model' kama kumbukumbu ya utumishi wake kwa watu aliofanya nao kazi
Tunakupongeza Mama Elizabeth Thomas kwa kuweza kutumikia vyema Halmashauri yetu kwa uadilifu na uaminifu, kwa heri Mama Thomas