Jiji la DSM Mabingwa wa UMITASHUMTA ngazi ya Mkoa kwa mwaka 2021

Na Hashim Jumbe TIMU ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, leo tarehe 31 Mei, 2021 wameibuka Mabingwa wa Jumla wa Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) ngazi ya Mkoa wa Dar es Salaam, yaliyofanyika kwa Siku Nne (4) katika viwanja vya Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) na uwanja wa Uhuru uliopo Temeke, Dar es Salaam.

 Mashindano hayo yaliyoshirikisha Timu Tano (5) kutoka katika Halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam ambazo ni Halmashauri ya Jiji la DSM, Manispaa ya Kinondoni, Ubungo, Kigamboni na Temeke yalifunguliwa tarehe 28 Mei, 2021 na kufungwa rasmi Siku ya leo na Afisa Elimu Mkoa wa DSM, Ndugu Abdul Maulid, huku Halmashauri ya Jiji la DSM wakiibuka washindi wa Jumla kwa kubeba vikombe Tisa (9) kati ya vikombe 16 vilivyoshindaniwa, ambapo Nafasi ya Pili ilienda kwa Manispaa ya Temeke.
Aidha, mashindano hayo yaliwakutanisha jumla ya wanamichezo 600 walioweka kambi Shule ya Sekondari Jitegemee, kama anavyosema Afisa Elimu Mkoa wa DSM, Ndugu Abdul Maulid "Natambua kuwa Halmashauri zote Tano (5) zimetoa washiriki 100 pamoja na walimu wao ni 120, hivyo hongereni kwa mkusanyiko mkubwa, mmekuwa hapa kwa Siku Nne (4) lakini katika Siku zenu 4 mmekuwa na nidhamu kubwa, kwa hiyo tunawashukuru sana Jitegemee kwa kutukaribisha na kutupa huduma tulizozitaka" Sambamba na Halmashauri ya Jiji la DSM kuwa Mabingwa wa Mkoa, lakini pia imeweza kutoa wachezaji wengi zaidi kwenda timu ya Mkoa wa DSM, wachezaji 72 kati ya wachezaji 120 wanaounda timu ya mkoa wa DSM itakayokwenda kushiriki michuano hiyo kwa ngazi ya Kitaifa, mashindano yatafanyika Mkoani Mtwara kuanzia tarehe 6 Juni, 2021 Itakumbukwa kuwa timu ya 

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ndiyo walikuwa Mabingwa watetezi wa michuano hiyo kwa Mkoa wa DSM na mwaka huu wameweza kutetea tena ubingwa wao na kuwa Mabingwa kwa Miaka Mitano (5) mfululizo

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi