Na;Rosetha Gange
Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam
Mhe.Amosi makalla leo tarehe 8/7/2021 amefanya ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya
ujenzi wa Machinjio ya kisasa ya Vingunguti na kutoa agizo kwa Mkandarasi wa machinjio
hayo ambaye ni Shirika la nyumba la Taifa (NHC) kuwa, mpaka kufikia tarehe 30/7
ujenzi uwe umekamilika ili tarehe 1/8 ianze kutumika rasmi.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe.Amos Makalla (katikati) akiongea na watendaji na wananchi wa Vingunguti
Akitoa taarifa ya ujenzi wa Machinjio hayo Mkurugenzi wa jiji la Dar es salaam Ndg.Jumanne Shauri amesema kuwa Halmashauri ya jiji la Dar es salaam ilisaini mkataba wa ujenzi wa Machinjio hayo na Shirika la nyumba la Taifa kwa gharama ya Sh.12.4Bil ambapo Sh.8.5 ni fedha kutoka Serikali kuu na Sh.3.9Bil ni mchango wa Halmashauri kutoka katika mapato yake ya ndani.
Aidha Ndg.Shauri amesema
kwamba mpaka sasa Mkandarasi wa Machinjio hayo amekwishalipwa kiasi cha Sh.Bil
9 hivyo kubakiwa na deni la Sh.Bil.3.3.Mpaka sasa ujenzi wa Machinjio hayo
umekwisha kamilika kwa 96% na wamejiwekea mpaka kufikia tarehe 1/8/2021
Machinjio hiyo ianze kutumika baada ya kukamilisha vitu vichache vilivyosalia
kama ujenzi wa mabucha ya kuuzia nyama,kukamilisha ujenzi wa tanki la
maji,kujenga banda la kuhifadhia ngozi pamoja na ujenzi wa chumba cha
kuhifadhia baridi (cold room).
Akisisitiza kauli ya Kazi
iendelee ya Mh.Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu
Hassan,Mhe.Makalla amesema kuwa mradi wa machinjio hayo ni mkubwa na muhimu
sana kwa nchi yetu hivyo ni lazima uanze kufanya kazi haraka ili serikali iweze kujipatia mapato na
matarajio yaliyolengwa na Serikali yaweze kutimia.
Mhe Makalla anasema,
“Mradi huu unakwenda kubadilisha maisha na uchumi wa watu.Pia ni mradi
ambao unakwenda kufungua fursa nzuri kwa mikoa mingine kwa sababu Dar es salaam
inategemewa sana katika soko la mifugo.Vilevile mradi huu utatoa fursa kwa
wafanyabiashara kupeleka nyama maeneo mengine kama Zanzibar,Comoro na
Dubai.Hivyo Mkandarasi fanya kazi usiku na mchana kukamilisha kazi iliyobaki.”
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe.Amos Makalla akipokea maelezo ya ufanisi wa Mashine mbalimbali katika machinjio hiyo.
Katika ziara ya ukaguzi wa Machinjio hayo Mhe.Makalla aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe.Ng’wilabuzu Ludigija,Meya wa Jiji la Dar es salaam Mhe.Omary Kumbilamoto,Mkurugenzi wa jiji la Dar es salaam Ndg.Jumanne Shauri na watendaji mbalimbali kutoka Halmashauri ya jiji la Dar es salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe.Amos Makalla na Wataalam mbalimbali wakipokea maelekezo kuhusu mfumo wa maji taka utakavyofanya kazi.
Mradi wa Machinjio ya kisasa
ya Vingunguti ulianza rasmi tarehe 8 Julai 2019 ukiwa unatekelezwa na
Mkandarasi ambaye ni Shirika la nyumba la Taifa (NHC) akisimamiwa na Mshauri
Mwenezi M/S CONS AFRIKA Ltd na FB Consultant wa Dar es salaam.