Karibu Mwenge Maalum wa Uhuru 2021 Wilaya ya Ilala

 Na: Hashim Jumbe

TAREHE 08 Desemba, 1961 muda mchache kabla ya kutimia Saa 6:00 Usiku, Luteni Alexander Gwebe Nyirenda alikuwa juu ya kilele cha Mlima Kilimanjaro akiwasha Mwenge, tukio ambalo lilikwenda sambamba na kupandishwa kwa bendera ya Taifa jipya la Tanganyika wakati bendera ya Uingereza ilipokuwa inateremshwa kwenye Uwanja wa Taifa wa Uhuru, Mkoani Dar es Salaam.

"Sisi tumekwisha uwasha Mwenge wa Uhuru na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike ndani na nje ya mipaka yetu, ulete matumaini pale ambapo hakuna matumaini, ulete upendo mahali penye chuki na heshima mahali palipo jaa dharau” maneno ya Mwalimu Nyerere wakati akitoa hotuba ya siku ya Uhuru, Tarehe 09 Desemba, 1961 akiwatangazia Watanganyika, Afrika na Dunia kwa ujumla

Aidha, baada ya Uhuru wa Tanganyika na kuwashwa kwa Mwenge wa Uhuru, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na viongozi wenzake walielekeza juhudi zao katika kuwaunganisha Watanzania na kuweka misingi imara ya kulijenga Taifa huru la Tanganyika, kudumisha amani, upendo, umoja, mshikamano na kuweka sera za kukabili maadui ujinga, umaskini na maradhi.

Itakumbukwa kuwa Mwenge wa Uhuru umekuwa ukikimbizwa Nchi nzima ukipita kwenye mitaa na umeendelea kuwakumbusha Watanzania wajibu wa kufanya kazi kwa bidii ili kuleta maendeleo huku ukitumika kuzindua miradi mbalimbali kila mwaka kwenye maeneo unakopita.

Kwa mwaka 2021 Mbio za Mwenge wa Uhuru ni Mbio Maalum na  umaalum wake pia unatokana na Mbio hizi za Mwenge wa Uhuru kukimbizwa kwa Siku 150 katika Wilaya 150 za kiutawala tu za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania badala ya Halmashauri za Wilaya 195 kama ilivyozoeleka

Kwa Wilaya ya Ilala, Mwege huo wa Uhuru utakimbizwa Tarehe 18 Agosti, 2021 na unatarajiwa kuzindua, kukagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo iliyotekelezwa, na moja kati ya miradi itakayotembelewa ni 'Kituo cha Mapato cha Buguruni' na kuonesha Wilaya ya Ilala inavyotumia kwa usahihi TEHAMA kuwahudumia Wananchi ipasavyo chini ya kaulimbiu ya Mwenge isemayo "TEHAMA ni msingi wa Taifa endelevu. Itumie kwa usahihi na Uwajibikaji”.


Karibu Mwenge Maalum wa Uhuru Wilaya ya Ilala, Wilaya iliyobeba sehemu kubwa ya Historia ya Mkoa wa Dar es Salaam, kwa maana ya vivutio na uzuri unaolifanya Jiji la Dar es Salaam kuwa miongoni mwa Majiji 10 yenye mvuto zaidi Barani Afrika, vivutio vilivyopo Ilala ni kama vile; Sanamu ya Askari, Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere, Ikulu ya DSM, Ukumbi wa Karimjee, Bandari ya DSM, Soko la Kariakoo, Viwanja vya Mashujaa Mnazi Mmoja, Kituo cha Reli ya DSM, Hospitali ya Muhimbili, Mnara wa Saa, Hoteli zenye hadhi ya Kimataifa, Soko la Samaki Feri, Benki Kuu ya Tanzania, Boma la Kale, Sekondari ya Pugu, Ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere

Pamoja na vivutio vyote hivyo kuwepo Wilaya ya Ilala, lakini pia shughuli mbalimbali za kibiashara hufanyika kwenye Wilaya hii inayoongozwa na Mhe. Ludigija, hivyo Ilala imeitambulisha DSM kuwa Jiji mashuhuri kwa biashara.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi