Mbio za Mwenge wa Uhuru 2021 zakagua Mradi wa Maji wa Mwaka 2019

 Na: Omary Omary

Mwenge Maalum wa Uhuru 2021 umekimbizwa katika Wilaya ya Ilala, Tarehe 18 Agosti, 2021 ambapo umepitia maeneo mbalimbali kwa ajili ya kueneza elimu juu ya mambo ya kijamii kama vile kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI, lakini pia kupitia miradi ya maendeleo ikiwa ni jitihada za kuhimiza uwajibikaji na uhamasishaji wa kufanya kazi kwa maendeleo ya ustawi wa nchi yetu.

 Mbio hizo zimeongozwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa 2021 Luteni Josephine Paul Mwambashi na moja kati ya miradi iliyokaguliwa ni ujenzi wa tanki la maji safi lenye uwezo wa kuchukua ujazo wa maji lita Milioni Mbili (2,000,000) lililopo Pugu Kajiungeni. Mradi huo ulipitiwa na Mwenge wa Uhuru mwaka 2019, hivyo Mwenge wa Uhuru 2021 ulipita kuangalia maendeleo ya mradi huo.

Aidha, taarifa ya mradi huo inaeleza kwamba, Mradi umekamilika kwa asilimia Mia Moja (100) ukiwa umetekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar-es-salaam (DAWASA), Mradi ulianzishwa Juni 2019, ukijengwa na  Kampuni ya CHIKO kutoka China na Mhandisi Mshauri wa Mradi ni Kampuni ya WAPCOS kutoka India. Mradi unahusisha usafirishaji wa maji safi kwa Wananchi kwa Kilomita 13.5 kutoka Kisarawe hadi Ukonga- Jijini Dar-es-salaam.

Sambamba na hilo mradi huo uliogharimu pesa za Kitanzania Shilingi Bilioni 7.3 mpaka kukamilika kwake, umeweza kunufaisha wakazi wa kata za Pugu, Gongolamboto, Chanika, Pugu-Machimbo, Pugu Stesheni, Pugu-Mnadani, Mongolandege, Ukonga, Kigogo Freshi, Bangulo, Buyuni, Kinyerezi na Ukonga Airwing kwa kuwezesha kuwasambazia maji safi na salama majumbani kwao.

Awali baadhi ya wananchi wa Kata ya Pugu na baadhi ya maeneo mengine ambayo sasa yamenufaishwa na mradi  walilazimika kutumia maji ya visima na wengine kusafiri umbali wa hadi nusu kilomita kwa ajili ya kuchota maji kwa matumizi ya kila siku ya nyumbani, hivyo basi tanki hili la maji limekuwa suluhisho la kero ya maji kwa wakazi wa maeneo hayo tajwa.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi