Na: Miraji Omary
Kiongozi wa Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru Kitaifa
2021, Luteni Josephine Paul Mwambashi, Tarehe 18 Agosti, 2021 alitembelea mradi
wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Ilala-Kasulu kwa ajili ya kuweka Jiwe la Msingi
katika Mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa ya ghorofa, ambao umegusa kigezo
cha nne (4) kipengele cha (4.5) kinachoonesha jinsi Wilaya ilivyo wekeza na
kusimamia miundombinu ya elimu. Mradi huo ambao ulianza Aprili 2019 na
unatarajiwa kukamilika Mwaka huu wa fedha 2021/2022.
Mkuu wa shule Bw. Hamisi Ernest Masutu akisoma taarifa
za mradi huo kwa kiongozi wa mbio maalum za Mwenge Luteni Josephine Paul
Mwambashi amesema kuwa mradi umetumia eneo dogo kutokana na ufinyu wa maeneo
katikati ya mji na kuwezesha kusajili Wanafunzi wengi, Kupunguza msongamano wa
wanafunzi darasani. Pia mradi umesaidia kuhudumia Watoto wa Kata zilizo karibu
hivyo kupunguza umbali wa Wanafunzi kwenda shule za pembezoni kitu ambacho
kimesaidia kuongeza ufaulu.
Aidha mkuu wa shule amesema wanaenda sambamba na
kaulimbiu ya Mwenge maalum wa Uhuru ya mwaka 2021, isemayo “Tehama ni Msingi wa Taifa Endelevu, Itumie kwa Usahihi na Uwajibikaji”
ambapo shule ya Sekondari Ilala Kasulu inatumia mifumo ya TEHAMA (PREMS, BEMIS,
NA FFARS) kwa baadhi ya shuguli, ambazo imerahisisha utendaji kazi kama vile
Usajili wa Wanafunzi, Uhamisho wa Wanafunzi, Uandaaji wa ripoti za Wanafunzi
pamoja na Shughuli za Uhasibu kama ilivyo kwa shule zingine katika Wilaya.
Pia mkuu wa shule ameongezea kwa kusema katika shule
ya Sekondari Ilala Kasulu, sekta ya elimu ipo mstari wa mbele katika mapambano
dhidi ya Rushwa kupitia kaulimbiu ya kudumu isemayo “Kupambana na Rushwa ni Jukumu Langu”, hivyo shule kwa kushirikiana
na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) imeanzisha Kikundi elimishi juu ya kupambana
na Rushwa mashuleni ili kujenga uelewa kwa vijana juu ya madhara yatokanayo na
kutoa au kupokea Rushwa.
Sambamba na hilo Kiongozi wa Mbio Maalum za Mwenge
Kitaifa 2021, Luteni Josephine Paul Mwambashi amezindua Klabu ya kupinga na
kupambana na Rushwa ya wanafunzi iliyoanzishwa kwa kushirikiana na TAKUKURU,
Baada ya taarifa iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa klabu Doreen Bernad, ambapo
amesema klabu hiyo inaundwa na wanachama wapatao 60, Wavulana 22 na Wasichana 38
wa Shule ya sekondari Ilala Kasulu.
Kiongozi wa Mbio Maalum za Mwenge Kitaifa 2021, Luteni
Josephine Paul Mwambashi, akihitimisha ziara yake katika mradi wa ujenzi wa
Shule ya Sekondari Ilala Kasulu, amewaasa viongozi wanao simamia miradi mbalimbali
kuweza kuonyesha nyaraka zote zinazo husiana na mradi husika pamoja na
kushirikisha wanchi wa eneo husika iliwaweze kutambua jinsi mradi unavyo
endeshwa.