Maafisa Mapato wapewa mafunzo ya ukusanyaji Mapato kwa mfumo wa kielektroniki

 Na Rosetha Gange

Maafisa mapato na wataalamu wa mfumo kutoka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam leo tarehe 29/10/2021 wamepewa mafunzo ya ukusanyaji mapato kwa kutumia mfumo wa kielektroniki unaojulikana kama GIS (Geographical Information System), mfumo ambao utawezesha kupata taarifa za kijiografia za wafanyabiashara na walipa kodi kwa kutumia vishikwambi maarufu kama Tablets.

Mafunzo hayo yaliyohudhuriwa na Maafisa TEHAMA kutoka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Maafisa Mapato, Maafisa Biashara,na Watumishi wengine wa Idara ya Frdha na Wanahabari kutoka Jiji la Dar es Salaam yamefanyika katika ukumbi wa Arnatouglo Mnazi Mmoja katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam

Akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Bi. Tabu Shaibu amewapongeza wawasilishaji wa mafunzo hayo kwa kazi nzuri wanayoifanya na kuwaomba washiriki wa mafuzo hayo kuyapokea mafunzo na kuwa tayari kuyafanyia kazi kwa vitendo,lengo ikiwa ni kuhakikisha Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inakusanya mapato kwa wingi na kufikia malengo iliyojiwekea kwa ufanisi zaidi.

Akipokea maagizo kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo, Mkuu wa Idara ya fedha na biashara Ndg. Tulusubya Kamalamo ametoa shukrani za dhati kwa Kaimu Mkurugenzi ambaye pia Kitengo cha TEHAMA kipo chini yake ambapo wamekuwa wakijitahidi sana kusimamia mifumo na kuwa wabunifu kwa kutunga sera na mikakati mbalimbali katika kuhakikisha matumizi ya TEHAMA yanazidi kuimarika katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaaam.

Aidha Ndg.Kamalamo amesema, “Sisi kama Idara ya fedha na biashara tumedhamiria kuhakikisha tunaleta mabadiliko makubwa katika nyanja ya ukusanyaji mapato.Pia tutajitahidi kuhakikisha kuwa hii mifumo ya kielektroniki na mifumo mingine ambayo ipo,iisaidie Halmashauri yetu kuongeza kiwango cha ukusanyaji mapato.”

Ndg.Kamalamo pia ametumia nafasi hiyo kuwapongeza watumishi wote wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kuwa kinara wa ukusanyaji mapato ya ndani ya Halmashauri kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba 2021 ikiwa ni robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2021/2022, na hii ni kufuatia taarifa iliyosomwa na Waziri wa TAMISEMI Mhe.Ummy Mwalimu jijini Dodoma mnamo 28/10/2021.

Afisa mapato wa Jiji la Dar es Salaam Ndg.James Bangu amesema kuwa yote yaliyojadiliwa na kuagizwa ameyapokea na kwa kushirikiana na watumishi wenzake watayafanyia kazi ipasavyo na kwa weledi mkubwa ili kufanikisha malengo yote na maazimio waliyojiwekea ya kuendelea kuwa vinara katika ukusanyaji mapato na kwa kiwango cha juu.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi