TASAF yatoa mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa Ugani Jiji la Dar es Salaam

Maafisa Ugani kutoka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam leo tarehe 14 Juni, 2022 wameanza kupatiwa mafunzo kupitia warsha iliyoandaliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii - TASAF. Mafunzo hayo yannatolewa kwa lengo la kuwajengea uwezo wa utendaji kazi maafisa hao ili waweze kusimamia na kutekeleza majukumu yao ya kunusuru kaya masikini kwa ufanisi.



Katika mafunzo hayo yanayofanyika katika ukumbi wa mikutano DMDP uliopo Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam, Afisa Mafunzo wa TASAF, Catherine Kisanga, amesema kuwa lengo kubwa la warsha za Jamii ni kuwajengea walengwa uwezo wa kuelewa taratibu za TASAF za kunusuru kaya masikini, kutambua majukumu yao na kutambua mpango huo unahitaji nini, hivyo kupunguza malalamiko yaliyokuwa yakitokea kwa wanufaika wa mpango huo.

 

Afisa Mafunzo kutoka TASAF Bi. Catherine Kisanga akitoa mafunzo kwa Maafisa Ugani wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam

“Kupitia mafunzo haya, maafisa hawa wataweza kuendesha warsha za jamii kwa tija zaidi na kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa na mpango huu kwa urahisi. Vilevile walengwa wa mpango huu wataelewa kwa urahisi wajibu na majukumu yao hivyo kupunguza malalamiko mengi yaliyokuwa yakitokea kwao”, amesema Kisanga.

Aidha, Mratibu wa TASAF kutoka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Marcella Msawanga, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuona bado kuna haja ya kuendelea kutekeleza mpango wa kunusuru kaya masikini kwa lengo la kupunguza umasikini kwa Watanzania.

 

Msawanga ameongeza kuwa kutokana na mafunzo hayo, Jiji la Dar es Salaam linatarajia wanufaika wa mafunzo hayo yanayotarajiwa kuisha tarehe 16 Juni 2022 watakwenda kubadilisha taswira nzima ya uelewa wa walengwa wa TASAF kuhusu kunusuru kaya masikini.


 

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi