Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’wilabuzu Ludigija, leo tarehe 13 Juni, 2022 amezindua kampeni ya “Kataa Kitaa” inayolenga kuwaondoa watoto wanaoishi mtaani ili wakaishi kwenye maeneo yaliyopangwa na Serikali. Kampeni hiyo ilizinduliwa katika eneo la Askari Monument lililopo Posta Mpya, Dar es Salaam.
Namshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassani, kwa kuimarisha huduma zinazotolewa kupitia vitengo vya maenedeleo ya jamii, jinsia, watoto na watu wanaoishi katika mazingira magumu. Kupitia kampeni hiyo tunaweza kuibadilisha jamii kwa kuweza kuwatumia watoto hawa kutoa elimu kwa watoto wengine ili wasiendelee kuishi mtaani,” amesema Ludigija.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya alikemia tabia ya baadhi ya wazazi kuwatumia watoto hao kama chanzo cha mapato kwa shughuli za kuomba omba mitaani. “Nakemea wazazi wote wanaotumia watoto hao wa mtaani kama chanzo chao cha mapato. Tabia hii inakwaza juhudi za Serikali za kuwaondoa watoto hao mitaani,” amesema Mkuu huyo wa Wilaya.
Kampeni hiyo inatekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kushirikiana na taasisi ya Pink Tie Foundation na James Foundation ambao ni wadau waliojitokeza na ushauri wa kuwasaidia watoto hao kupata sehemu za kuishi, kujua vipaji vyao na mahitaji yao.
Mwakilishi wa taasisi ya Pink Tie Foundation, Lilian Mwasha alisema taasisi yao ilikusanya nguvu za kuwakutanisha watu mbali mbali kwa lengo la kuwasidia watoto hao ikiwa ni pamoja na kutoa msaada wa kisheria.
Akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari, Mawasiliano na Uhusiano, Tabu Shaibu, amesema Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kupitia kitengo chake cha Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na taasisi ya Pink Tie foundation inauunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kuwasaidia na kuboresha ustawi wa watoto.