Waheshimiwa Madiwani na Watendaji kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe wafanya ziara ya kimafunzo Jiji la DSM

Jiji la Dar es Salaam limepokea ujumbe wa Viongozi na Watendaji kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe iliyopo mkoani Mbeya, waliofanya ziara ya kujifunza mbinu mbalimbali za ukusanyaji wa mapato, usafi wa mazingira na Usimamizi wa Miradi pamoja na kutembelea Soko la Kimataifa la Samaki Feri kujifunza uendeshaji wa masoko.


Ujumbe huo uliongozwa na Mkuu wa Wilaya Rungwe Mhe. Jaffar Haniu ambaye amewashukuru viongozi na watendaji wa Jiji la Dar es Salaam kwa mapokezi mazuri na kukubali kuwapatia mafunzo hayo na kuwapongeza kwa ukusanyaji wa mapato.

Akiongea wakati wa kufungua mafunzo hayo yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Arnatoglou, Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam Ojambi Masaburi amesema “Nachukua nafasi hii kuwakaribisha katika Jiji la Dar es Salaam na tumefarijika kupokea ugeni huu mkubwa kutoka Rungwe hii inatupa uwezo wa kubadilishana uzoefu, sisi tuwape yetu lakini pia tupokee kutoka kwenu.”


Nae Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe Mpokigwa Mwankuga amesema kuwa wamejifunza mambo mengi mazuri ambayo hapo awali walikuwa hawayafahamu hivyo kwa namna moja au nyingine yatabadilisha utendaji wao wa kazi na kuleta matokeo chanya katika Halmashauri yao.

Tumejifunza mambo mengi ambayo tulikuwa hatuyafahamu hapo awali. Tumejifunza mbinu hasa uanzishwaji wa kanda katika kusimamia na kukusanya mapato na usafi wa mazingira . Nina imani haya yote tuliyojifunza tukiyaweka kwenye utekelezaji tutakuwa tumepiga hatua kubwa.” amesema Ndg. Mwankuga.


Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imekuwa ikipokea wageni mara kwa mara kutoka ndani na nje ya nchi wanaokuja kujifunza namna inavyotekeleza majukumu yake na kupata mafanikio makubwa katika nyanja mbalimbali kama ukusanyaji mapato.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi