KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, CPA Amos Makalla, ameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
CPA Makalla amebainisha hayo leo Julai 8, 2024 Jijini Dar es Salaam, akiendelea na ziara yake katika Jimbo la Segerea ambapo alitembelea mradi wa ujenzi wa ghorofa 20 Shule ya Sekondari Minazi Mirefu wenye thamani ya shilingi bilioni 1.79 pamoja na Mradi wa Kituo cha Afya Kinyerezi chenye thamani ya shilingi milioni 500.
Akiwa kwenye ziara hiyo, CPA Makalla Ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa utekelezaji mzuri wa miradi kwani thamani ya fedha inaonekana na miradi imetekelezwa kwa kiwango cha juu.
“Niwapongeza Mkuu wa Wilaya ya Ilala kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Jiji kwa utekelezaji wa miradi kwani Jitihada za Serikali za kuboresha huduma kwa wananchi zinaonekana pia mmeweza kutekeleza miradi hii kwa kutumia fedha za mapato ya ndani na nyingine za Serikali kuu hizi ni jitihada nzuri mnazozifanya za kuendelea kuboresha huduma za afya na Elimu kwa Wananchi wa Jiji la Dar es Salaam."
Sambamba na hilo, CPA Makalla amemshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuhakikisha sekta za Elimu na Afya zinaboreshwa na huduma zinawafikia wananchi kwa Wakati huku akiwataka Waganga Wafawidhi kuhakikisha huduma zinaboreshwa kwa Wananchi kwa kuwatia moyo na kuhakikisha majengo mazuri yananendana na huduma bora.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo ameeleza kuwa “Tunatoa Shukrani zetu kwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha huduma za elimu na afya katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwani fedha nyingi zimekua zikiletwa kwaajili ya kuboresha miundombinu ya afya na elimu lengo likiwa ni kuhakikisha sekta hizo zinakua imara na wanachi wanapata huduma bora na kwa wakati."
Aidha, Mhe. Mpogolo ameendelea kusema Serikali imeendelea kuwekeza katika sekta ya Elimu na Afya kwani katika Jiji la Dar es Salaam Shule za ghorofa zaidi ya 8 zinaendelea kujengwa zikiwa katika hatua mbalimbali hii itasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani na kuongeza ufaulu zaidi.