Na: Hashim Jumbe
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija, leo tarehe 01 Julai, 2022 amefungua rasmi mashindano ya umoja wa michezo na taaluma kwa shule za msingi Tanzania, maarufu kama UMITASHUMTA kwa ngazi ya Wilaya ya Ilala.
Mashindano hayo yanayofanyika kwa siku 3 kwenye viwanja vya Shule ya Kebby vilivyopo Pugu Kinyamwezi, yalianzia kwa kushindanishwa timu za madarasa, shule, kata na hatimaye kufikia kutengeneza timu za Klasta, ambazo leo zimeanza kushindanishwa ili kutengeneza timu itakayowakilisha Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwenye ngazi ya UMITASHUMTA Mkoa.
"Mheshimiwa Mgeni rasmi, mbele yako ni wanamichezo 480 pamoja na walimu wao kutoka Klasta za Chanika, Ukonga, Kimanga na Gerezani ambao leo wanaanza rasmi Mashindano ya UMITASHUMTA ngazi ya wilaya. Mashindano haya yanashirikisha michezo ya wavu, soka, riadha, netboli, mpira wa mikono, ngoma na kwaya" alisema Bi. Asha Mapunda ambaye ni Afisa Elimu Michezo wa Idara ya Elimu Msingi Jiji la Dar es Salaam
Naye Afisa Elimu Msingi Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Bi. Sipora Tenga akiongea wakati akimkaribisha Mgeni rasmi alisema "Wilaya yetu imekuwa ikifanya vyema sana katika mashindano ya UMITASHUMTA na hata taaluma. Mwaka 2021 tuliweza kupata nafasi ya kwanza kitaifa kwa upande wa ngoma na nafasi ya 8 upande wa kwaya, pia tuliweza kutoa idadi kubwa ya wachezaji 72 kati ya 100 ambao ni sawa na 70% kwa waliounda timu ya Mkoa wa Dar es salaam"
Mashindano ya UMITASHUMTA kwa mwaka 2022 yanabeba kauli mbiu isemayo “TAKWIMU SAHIHI NI MSINGI WA MIPANGO BORA YA TAIFA” SHIRIKI SENSA YA WATU NA MAKAZI KWA MAENDELEO YETU.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala wakati akifungua mashindano hayo aliwakumbusha wanafunzi hao lengo la wao kuwepo hapo "lengo la mashindano haya ni kushindanisha wanafunzi katika michezo mbalimbali ili kuibua vipaji vya vijana watakaounda timu bora ya wilaya na baadaye kushiriki mashindano ya UMITASHUMTA Mkoa wa Dar es salaam, niwaase kucheza kwa juhudi ili tupate timu itakayokwenda kushindana ngazi ya Mkoa na kuibuka washindi, siku zote Ilala sisi ni washindi" Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija
Ikumbukwe kuwa timu ya Wilaya ya Ilala ndiyo inayoshikilia ubingwa wa UMITASHUMTA kwa ngazi ya Mkoa wa Dar es Salaam kwa miaka minne (4) mfululizo, hivyo kuwa na nafasi nzuri kwa mwaka huu kushinda kwa mara ya tano (5) mfululizo.