Na: Hashim Jumbe, Mkoani Tabora
Walimu Wakuu wa Shule za Msingi za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, leo tarehe 05 Agosti, 2022 wameitembelea kambi ya wanafunzi wa UMITASHUMTA Mkoa wa Dar es Salaam wanaoendela na mashindano ya 22 ya UMITASHUMTA yanayofanyika hapa Mkoani Tabora.
Walimu hao Wakuu wamekutana na timu hiyo na kuwapa hamasa wanafunzi hao kuelekea michezo yao ya kesho ambapo timu ya Mkoa wa Dar es Salaam imefuzu hatua ya robo fainali kwa mpira wa miguu wavulana, nusu fainali mpira wa miguu maalum (wanafunzi viziwi) nusu fainali mpira wa wavu wasichana na mchezo wa fainali fani za ndani kwenye ngoma na kuimba pamoja na riadha raundi ya tatu (3)
"Tumekuja kuwapa hamasa ili mpate nguvu ya kutengeneza matokeo yaliyo mazuri zaidi ya yale ambayo yamepatikana, sisi Walimu Wakuu ambao ni wanachama wa TAPSHA Jijini Dar es Salaam tumeamua kutoa kwenu huduma ya chai na chakula Siku ya Jumapili" Mwl. Simon Mndendemi, Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Mikongeni
Pamoja na ahadi hizo, lakini pia Shule za Kingereza za Serikali za Jiji la Dar es Salaam nazo zimetoa ahadi kwa wanafunzi hao "kwa niaba ya Shule ya Diamond, Olympio na Mikongeni tunatoa ahadi ya Shilingi Laki Tatu kwa ajili ya maji" Mwl. Mndendemi