Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija leo tarehe 9 Disemba, 2022 ameshiriki kwenye mdahalo kujadili maendeleo mbalimbali yaliyopo katika Wilaya ya Ilala tangu kupatikana kwa Uhuru wa Nchi yetu hadi sasa.
Mdahalo huo umefanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Karimjee ikiwa ni Siku ya Maadhimisho ya Miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania Bara ambapo Mkuu wa Wilaya ya Ilala kwenye hotuba yake alisema "Katika miaka 61 ya Uhuru Ilala imefikia maendeleo makubwa sana ukiangalia Sekta ya Elimu hapo mwanzo Dar es Salaam kulikuwa na Shule Tano tu na zote zilikuwa Chini ya Wakoloni leo hii Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam katika Uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuna jumla ya Shule 106 ndani yake shule 60 ni za Serikali na shule 41 ni shule Binafsi, haya ni mafanikio makubwa sana katika Sekta ya Elimu"
Aidha, Mhe. Ludigija alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia kwa kuipatia Wilaya ya Ilala fedha za ujenzi wa mabweni maalum "Namshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kutoa pesa katika hizi ambazo kila miaka zinatumika katika sherehe za maadhimisho ya Uhuru na sasa zimeenda kujenga Mabweni ya shule Maalumu". Amesema Mhe. Ludigija.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija akiwa na wanafunzi waliohudhuria kwenye mdahalo huo |
Katika mdahalo huo mada mbalimbali zimewasilishwa kama vile kuhusu Elimu kutoka Uhuru hadi sasa, Siasa toka uhuru hadi sasa, uchumi na maendeleo kutoka Uhuru hadi sasa pamoja na kutathmini maendeleo katika miaka 61 ya uhuru wa Tanzania bara.
Akiwasilisha mada ya siasa na maendeleo Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam amesema "Tuenzi maneno ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere lakini pia kupitia maadhimisho haya Mkuu wa Wilaya mpelekee salamu zetu Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa Pesa Shilingi Bilioni 6.2 kwa ajili ya Ujenzi wa vyumba vya madarasa na naomba aendelee hivi hivi kwa miaka iliyobakia ili pesa ambazo zilikuwa zinafanya sherehe hizi kitaifa ziende katika kuimarisha shughuli za maendeleo kwa kila Wilaya"
Katika kuimarisha siasa safi toka kipindi tunapata Uhuru tukiwa na chama kimoja hadi sasa Tanzania tuna jumla ya Vyama vya Siasa 22 vilivyosajiliwa kwa kudumu hii ni ishara yakuwa na siasa safi inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita ikiwepo pia kuwatoa wanasiasa walioko magerezani kurudi uraiani na kufanya siasa.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Wilaya ya Ilala Mzee Matimbwa wakati akifanya wasilisho amesema "Kabla ya Uhuru hatukuwa na Chuo kikuu bali vyuo vilianza kupatikana kwa kuchangia kutoka kwa wananchi na kwa sasa tunaona namna Rais Dkt Samia Suluhu Hassan anatoa pesa kujenga madarasa kuendeleza elimu katika kuhimiza hilo kuwa misingi ya uongozi bora ni uaminifu na uzalendo wa kweli kwa kujali maslahi ya Nchi na ukiwa mzalendo na uzalendo ukiwepo hakutokuwa na rushwa kama tukiwa wazalendo tutaitekeleza siasa safi na nachukua nafasi hii kumpongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuenzi mambo yote kutoka wakati wa uhuru hadi leo kwa kusimamia kila zuri toka uhuru hadi sasa"
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija akikabidhi zawadi ya mbuzi kwa washindi wa mpira wa pete waliopatikana kwenye bonanza ya kusherehekea Uhuru lililofanyika 8 Disemba, 2022 |
Mdahalo wa maadhimisho ya Miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania Bara uliofanyika katika ukumbi wa Karimjee ulitanguliwa na matukio mbalimbali wakati wa juma la kilele cha Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 61 ya Uhuru, matukio hayo ni pamoja na zoezi la upandaji miti katika Wilaya, mashindano ya Insha, usafi wa mazingira na shughuli za Kijamii, bonanza la michezo pamoja na mahojiano maalum na wazee huku maadhimisho hayo yakibeba kaulimbiu isemayo “Amani na Umoja ni Nguzo ya Maendeleo yetu”