Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Ng’wilabuzu Ludigija amewataka wafanyabiashara wote wakiwemo wafanyabiashara ndogondogo maarufu Kama Machinga kuingia kwenye 'Data base' ya TRA lengo likiwa ni kuepusha risiti feki zinazotolewa na wafanyabiashara hao.
Hayo ameyabainisha leo Disemba 5, 2022 wakati wa ziara yake ya kuongea na wafanyabiashara ndogondogo iliyofanyika katika soko la Kariakoo Jijini Dar es Salaam.
Aidha, Mhe. Ludigija amewataka wafanyabiashara hao kubandika bango dogo katika milango ya maduka yao lengo likiwa ni kuwakumbusha wateja wanaoingia kwenye maduka waweze kuona na kuhakikisha wanapewa risiti zenye TIN Namba sawa naitakavyoonekana kwenye bango hilo.
“Wafanyabiashara wote wa maduka tuhakikishe tunabandika mabango haya kutoka TRA ili tuwakumbushe wateja wetu wanapoingia dukani kununua bidhaa na apewe risiti sawasawa na ile inayoonekana kwenye stika hii ni kutokana na kwamba kumekuwepo na risiti za EFD feki hivyo kutokana na mpango huu wa kubandika stika ili kuwakumbusha wateja wanapopewa risiti kuangalia Kama iko sawasawa na kwenye stika itasaidia sana kupunguza utoaji wa risiti feki kwani risiti nyingi zilizokua zikitolewa zikihakikiwa kwenye mfumo zinaonekana ni feki hii ndiyo sababu kubwa ya kuanzisha utaratibu huu ili kuepuka utoaji wa risiti zisizo halali” Ameeleza Mhe. Ludigija.
Sambamba na hilo Mhe. Ludigija ameendelea kusema ”Kimsingi EFD machine hizi ilikua tuzinunue sisi lakini meneja wa TRA atakavyowakadiria malipo ya awali yatatumika kwa wafanyabiashara kununua hizo EFD machine”.
Aidha Mhe.Ludigija amewataka wafanyabiashara ndogondogo kuhakikisha wanajipanga vizuri kama walivyopangwa hapo awali “Mimi kama Mkuu wa Wilaya kazi yangu mimi ni kuhakikisha kila mfanyabiashara hafungi biashara yake na pia sipendi kuona au kusikia mfanyabishara kafungiwa biashara kwasababu hajalipia EFD machine hivyo nitoe wito kwa wafanyabiashara wote na maafisa wote kuwa elimu itaendelea kutolewa kwa wafanyabiashara hao na Meneja uhakikishe wafuatiliaji wa suala hili hawatengenezi manyanyaso kwa wafanyabiashara hawa lengo likiwa ni kuendelea kukuza pato la Taifa letu.”