Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ipo kwenye utekelezaji wa mpango wa ujenzi wa vyumba vya madarasa 310 kwa Shule za Sekondari kupitia fedha zilizotolewa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan maarufu kama 'Pochi ya Mama'
Aidha, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, imepokea Jumla ya fedha Shilingi Bilioni 6.2 kwa ujenzi wa vyumba vya madarasa 310 huku kila chumba kikijengwa kwa fedha Shilingi Milioni 20
"Katika madarasa hayo tunajenga vyumba vya madarasa ya msambao 273 na madarasa ya ghorofa 37 yanayojengwa Shule ya Sekondari Kipunguni, madarasa 16, Shule ya Sekondari Minazi Mirefu madarasa 05, Shule ya Sekondari Liwiti madarasa 09 na madarasa 07 yanajengwa Shule ya Sekondari Mnazi Mmoja" Mwl. Mussa Ally, Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Ujenzi wa vyumba vya madarasa 37 ya ghorofa umezingatia ufinyu wa maeneo ambapo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeweza kutoka Shilingi Milioni 800 kufanikisha ujenzi huo
"Katika Shule 04 zinazojengwa madarasa ya ghorofa, Halmashauri imepeleka Shilingi Milioni 200 kwenye kila Shule sawa na Milioni 800, lengo ni kuhakikisha kwamba maeneo hayo finyu ambayo baadhi yao kwa mwaka jana tulilazimika kuhamisha madarasa kupeleka sehemu yenye nafasi, mwaka huu yatajengwa katika mtindo wa ghorofa kwa ku 'support' na fedha za Halmashauri" Mwl. Mussa Ally
Kazi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 310 inatarajiwa kukamilika kwa wakati ili vyumba hivyo viweze kutumiwa na wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2023.
"Sisi tunajipanga kukamilisha madarasa yetu ndani ya muda uliopangwa na kufanya hivyo tumeunda timu za usimamizi ziko huko katika mashule na tumewahusisha pia Wakuu wa Idara mbalimbali kama walezi na sisi wenyewe tunazunguka kuangalia" Mwl. Mussa Ally
Itakumbukwa kwamba wanafunzi Elfu 30 wamehitimu elimu ya msingi kwa mwaka 2022 kwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, hivyo kufanya upungufu wa vyumba vya madarasa ya kusomea kidato cha kwanza mwaka 2023 kufikia 310, hali hiyo imeilazimu Serikali kutoa fedha kujenga vyumba hivyo vya madarasa
"Tulikuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa 310 ambapo kwa hakika madarasa yote 310 yamepatikana, na makisio yetu Halmashauri ni kwamba ufaulu utaongezeka, watoto wote Elfu 30 watakaokuwa wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2023 watapata nafasi ya kusoma" Mwl. Mussa Ally