Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Ilala wafanya ziara Idara ya Elimu Sekondari Jiji la DSM

Katibu wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala ameridhishwa na mwenendo wa utekelezaji wa Ilani ya Chama kwa upande wa Idara ya Elimu Sekondari katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, hayo ameyabainisha leo Januari 17, 2023 katika ziara yake na wajumbe wa kamati ya utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi ya CCM Wilaya ya Ilala walipojadiliana mambo mbalimbali kuhusu namna ya kuboresha Elimu ya Sekondari, Vyuo vya Elimu ya Juu na Vyuo vya Ufundi ikiwepo Elimu ya Watu Wazima.

Akiongea katika ziara hiyo Katibu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Wilaya ya Ilala Ndugu Mtiti Mbassa Jirabi ameeleza kuwa "Lengo la kuja hapa ni kuhakikisha tunapata maelezo sahihi na ya kina kama sehemu ya kujifunza ili tukatoe elimu kwa wanachama wetu wa Jumuiya ya Wazazi inayosimamia Elimu, Malezi, Mazingira, Afya pamoja na Utamaduni.


Aidha, Ndugu Mbassa aliendelea kusema “Kama kamati ya utekelezaji tunaridhishwa na mwenendo wa Elimu katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, lakini pia ombi letu kubwa tunaomba utoro mashuleni ushughulikiwe pamoja na mwenendo wa maadili kwa wanafunzi wa rika huku tukiwataka wanafunzi wenye mahitaji maalumu kupewa kipaumbele ili waweze kusoma katika mazingira rafiki kama wanafunzi wengine.

Naye Afisa Elimu wa Sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Mwl. Mussa Ally amesema “Kipekee napenda kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuboresha sekta ya Elimu Nchini kwani amekua akifanya jitihada za juu sana kuhakikisha anatoa fedha kwaajili ya ujenzi wa madarasa lengo likiwa ni kuhakikisha wanafunzi wote wanaofaulu kwenda Sekondari waweze kusoma katika miundombinu rafiki ili kukuza sekta ya elimu nchini.


Sambamba na hilo Mwl. Mussa ameeleza kua katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi ibara ya 80 kipengele ‘A’ inaangalia watoto wa Tanzania wote wenye uhitaji wa kupewa elimu wapewe fursa na Elimu hiyo iwe bora na yenye mafanikio kwa watoto wetu hivyo kutokana na kifungu hicho, Halmashauri ya Jiji la DSM kupitia Idara ya Elimu Sekondari wameweza kutekeleza hilo.

Niwahakikishie tu kwamba kutokana na utekelezaji wa Ilani ya Chama sisi kama Idara ya Elimu Sekondari tutahakikisha wanafunzi wanasoma kwa bidii katika mazingira rafiki na pia tutahakikisha tunaukomesha utoro kwa kushirikiana na viongozi wote kuanzia ngazi ya Kata pia hatutaishia humo kwani kwa watoto watakaopata mimba mashuleni wataendelea na masomo kwa kuendelea kusoma elimu ya watu wazima hivyo niwahakikishie tu yakwamba watoto wetu watasoma kwenye mazingira salama na ufaulu utazidi kuongezeka.” alimalizia Mwl. Mussa

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi