Watendaji wa Sekta ya Elimu Jiji la DSM watakiwa kupandisha ufaulu, huku wakisaini mikataba ya uwajibikaji

Watumishi wa Idara ya Elimu Msingi na Idara ya Elimu Sekondari Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, leo tararehe 16 Januari, 2023 wamefanya kikao kazi cha pamoja katika ukumbi wa Shule ya Msingi Mnazi Mmoja, lengo likiwa ni kuboresha Sekta ya Elimu ili wanafunzi waweze kupata elimu katika mazingira mazuri ambayo yatapelekea kupandisha ufaulu wao.


Kikao hicho kiliwahusisha Walimu Wakuu wa Shule za Msingi za Serikali, Wakuu wa Shule za Sekondari za Serikali, Waratibu wa Elimu Kata na Maafisa Elimu kutoka Idara za Elimu za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, ambapo Mkuu wa Wilaya ya Wilaya Ilala, Mhe. Ludigija alitumia fursa hiyo kuwataka Watendaji katika Sekta ya Elimu kufuata maelekezo yaliyoelekezwa na Serikali ikiwa ni pamoja na mahudhurio, ufundishaji na ufundishwaji kuwa na mikakati na mbinu katika kutekeleza hayo kwani lengo la Serikali ni kuhakikisha kila mtoto anakuwa Shuleni na kupata matokeo chanya.


Sambamba na hilo lakini pia Mkuu wa Wilaya ameagiza Wakuu wa Shule za Sekondari kuhakikisha Wanafunzi wote waliopangwa Katika Shule zilizopo Wilaya ya Ilala wanaripoti huku akiwapongeza Wakuu wa Shule za Sekondari kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa madarasa “Niwapongeze Wakuu wa Shule za Sekondari kwa usimamizi mzuri wa ujenzi vyumba vya madarasa, kwa kweli mmejitahidi kuendana na kasi na madarasa yamejengwa kwa ubora unaotakiwa” Amesema Mhe. Ludigijja.

Naye, Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Mwl. Musa Ally amesema matarajio yao ni kuhakikisha maelekezo yote yaliyotolewa kwenye Vigezo vya Utendaji vinafikiwa kwa Asilimia 100 na kuhakikisha miundombinu katika Sekta ya Elimu kama madarasa, matundu ya vyoo, maabara, mabweni inaimarika.


Vilevile Sekta hiyo ya Elimu imejipanga kuhakikisha ufaulu katika Halmshauri hiyo unapanda kutoka asilimia 35 mpaka asilimia 50 na zaidi, wanafunzi wa Kidato cha Nne kufaulu kwa daraja la Kwanza, Pili na Tatu kwa ufaulu wa A, B, C sambamba na udahili na mahudhurio vifikie asilimia 100.

Lengo letu ni kufanya yasiyowezekana yawezekane kwa kuhakikisha miundombinu katika Sekta ya Elimu inaimarika na mazingira mazuri yote yanayofanya mwanafunzi kuweza kusoma vizuri yanafanyika” Amesema Mwl. Mussa Ally.

Akizungumza katika Kikao hicho Afisa Elimu Msingi Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Mwl. Sipora Tenga amesema kupitia kikao hicho watahakikisha kila Afisa Elimu wa Kata na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam awajue wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika na kuwapeleka katika hatua nzuri kulingana na Kata zao lakini pia watahakikisha Walimu wanaofundisha Darasa la Tatu wanakuwa mahiri katika somo la Kiingereza ili kuwajengea Wanafunzi wa Darasa la Tatu umahiri wa lugha ya kiingereza.

Sambamba na hayo kikao hicho pia kiliambatana na kusaini kwa mkataba wa Uwajibikaji na Utendaji Kazi kwa Maafisa Elimu Kata, Walimu Wakuu wa Shule za Msingi na Wakuu wa Shule za Sekondari ndani ya Halmshauri hiyo.




Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi