Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kupitia Kitengo chake cha TEHAMA imetoa mafunzo ya matumizi ya vishikwambi kwa Waheshimiwa Madiwani yenye lengo la kuwawezesha kuulewa mfumo wa ‘DCC Online Minutes’ ambao utarahisisha utendaji kazi kwa kupunguza matumizi ya makaratasi.
Akizungumza kwenye mafunzo hayo yaliyofanyika leo tarehe 11 Januari, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Arnatoglou, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Mhe. Omary Kumbilamoto amesema kuwa Halmashauri imejipanga kwa kumuwezesha kila Diwani kupata kishikwambi chake na kuwa vishikwambi hivyo vinakwenda kurahisisha utendaji kazi kwa Waheshimiwa hao kwani watafanya kazi kulingana na teknolojia ya kisasa na kuondokana na mfumo wa zamani wa kubeba makabrasha. “Niwapongeze sana Kitengo cha TEHAMA kwani mfumo huu utakwenda kupunguza adha ya kuhangaika na makaratasi. Vilevile matumizi ya mfumo huo utakwenda kuokoa muda kwani taarifa zitafika kwa wakati, na pia yatapunguza gharama.” Amesema Mhe. Kumbilamoto.
Naye Afisa Utumishi Bi. Benadeta Mwaikambo amesema mafunzo hayo yatawapa weledi Madiwani na kuwasaidia kufanya kazi kwa ufanisi.