Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija amewahakikishia wananchi wa Jiji la Dar es Salaam kumaliza changamoto ya kujaa maji iliyojitokeza katika Barabara ya Nyerere eneo la Kamata katikati ya Jiji.
Akizungumza alipotembelea Barabara ya Nyerere, Mhe. Ludigija amesema tayari ameshachukua hatua za haraka kwa kuwaelekeza wataalamu kutoka TANROADS kuchukua hatua za awali ili kutoa suluhisho la maji hayo kwa muda mfupi na muda mrefu.
Aidha, Mhandisi wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam, Kitengo cha Miradi ya Maendeleo, Bi. Mwanaisha Rajabu amewahakikishia wananchi wa Jiji la Dar es Salaam kwamba TANROADS itaenda kumaliza changamoto hiyo ikiwa ni suluhisho la kudumu kupitia mradi wake BRT awamu ya tatu. "Kwa hiyo suluhisho la kudumu tutalipata wakati wa ujenzi wa Mradi wa BRT awamu ya tatu, una kipengele cha kurekebisha miundombinu ya maji eneo hili, tayari mkandarasi ameshapatikana na yupo saiti". Amesema Bi. Mwanaisha.
Mhe. Ludigija pia ametoa maelekezo kwa taasisi zote za Serikali zinazoshugulika na barabara kupita na kukagua barabara zote ndani ya Wilaya ya Ilala na hasa katikati ya Jiji na kuhakikisha wanazibua mifereji yote ya maji.