Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija, leo tarahe 06 Januari, 2023 amezindua Madarasa 10 yaliyokamilika katika Shule ya Sekondari Nguvu Mpya iliyopo Chanika Jijini Dar es Salaam, madarasa hayo ni miongoni mwa madarasa 310 yaliyojengwa kwa fedha ya Pochi la Mama, ambapo shule hiyo ilipokea kiasi cha Shilingi Milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa hayo 10, ofisi ya Walimu na ununuzi wa viti na meza.
Katika uzinduzi huo Mh. Ludigija amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu kwa kuipatia Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kiasi cha Shilingi Bilion 6.2 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 310 "Namshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea kiasi cha shilingi bil 6.2 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 310, kuanzia Jumatatu ambapo shule zinaenda kufunguliwa hakuna mtoto kwenye Halmashauri yetu ya Jiji la Dar es Salaam atakayeshindwa kuingia shuleni kwa sababu ya madarasa, Mama amefungua pochi na pochi lenyewe ndilo hili linaonekana” Amesema Mhe. Ludigija.
Naye Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Mhandisi Amani Mafuru amesema Halmashauri imejipanga kwa kutenga kiasi cha Shilingi Milioni 700 kwa ajili ya kufidia idadi ya madawati yaliyopungua. Vilevile itatumia mapato yake ya ndani kwa kujenga matundu ya vyoo kulingana na idadi ya ongezeko la wanafunzi kwa shule zilizopo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Mhandisi Mafuru amemuhakikishia Mkuu wa Wilaya wa Ilala kuwa kila mtoto atakaa kwenye kiti na meza yake.
Naye Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Mhe Jerry Silaa, ametoa pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani fedha za Pochi la Mama zimesaidia wananchi hasa wanafunzi wa Jimbo lake kwa ujenzi madarasa ya shule zilizopo Jimbo la Ukonga, ambapo Jimbo hilo peke yake limepokea kiasi Shilingi billion 4.6. “Nitoe pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais kwani Jimbo la Ukonga limependelewa tumepokea kiasi cha shilingi billion 4.6 na siyo kwamba limependelewa ni kwa sababu lina idadi kubwa ya watu.” Amesema Mhe. Silaa
Akihitimisha Mkuu wa Shule ya Sekondari Nguvu Mpya, Bwana.Daniel Mwakyambiki amewataka walimu kuwa waadilifu na waaminifu wanapopokea fedha kwa ajili ya ujenzi kwa kufuata sheria na taratibu.