Wafadhili kutoka Demeter Financial & Insurance Services na Lions Club of DSM leo tarehe 22 Desemba, 2022 wametoa msaada wa madawati kwa Shule ya Msingi Yongwe iliyopo Kata ya Chanika ikiwa ni sehemu ya mchango wa wadau wa elimu kuhakikisha elimu kwa watu wote linatimia.
Akiongea katika hafla hiyo Muwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Bi. Tabu Shaibu aliwashukuru na kuwaahidi kuendelea kushirikiana na wadau hao.
“Halmashauri iko tayari kushirikiana na wadau wa maendeleo na nitahakikisha kuwa yote ambayo ni muhimu zaidi yatatekelezwa kwa wakati.
Nawashukuru sana wadau kwa kuweza kuwa sehemu ya kuipeleka mbele elimu. Demeter mmetoa madawati 53 na Lions Club mmetoa mawadati 55 ambayo yataenda kuwasaidia wanafunzi hawa moja kwa moja. Kwa hakika nyie ni marafiki wa kweli wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam hatuwezi kuwalipa” alimalizia Bi. Tabu Shaibu
Akiongea kwa niaba ya wadau hao Mkurugenzi Mtendaji wa Demeter Financial & Insurance Services Ndg. Adarsh Sharma amesema “Nina furaha sana kuwa hapa na kutoa madawati kwa ajili ya wanafunzi na naahaidi kuwa tutaendelea pamoja na mpaka mwisho na naitakia kila la kheri shule na wanafunzi”
Nae Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Yongwe Mwl. John Sendeu amesema “Tunashukuru sana Mkurugenzi na tunafuraha na ujio wako katika hadhira hii leo tunafuraha kupata madawati haya 108 kwa kiwango kikubwa tumepunguza sana uhitaji wa madawati katika shule hii ya Yongwe yenye jumla ya wanafunzi 1511.
Pia tunaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndani ya miaka hii miwili Mhe. Dkt. Samia Suluhu ametujengea matundu ya vyoo 10 na kwa sasa pia tunaendelea na ujenzi mwingine wa matundu 10 ya choo.” Alimalizia Mwl. Sendeu