Magonjwa ya mlipuko ni magonjwa ambayo hutokea kutokana na maambukizi ya ugonjwa fulani na kwa kawaida huenea haraka na kuathiri watu wengi kwa kipindi cha muda mfupi katika eneo fulani.
Mfano wa magonjwa ya mlipuko ni kama Kipindupindu, UVIKO 19, Ebola, Dengue, Mafua ya ndege n.k.
Kutokana na tafiti zilizofanywa na wataalamu mbalimbali wa masuala ya afya ndani na nje ya nchi vyanzo vikuu vya magonjwa ya mlipuko huwa ni kutumia maji yasiyo safi na salama yenye vimelea vya bakteria ndani yake, mabadiliko ya majira katika mwaka yaani vipindi vya joto kali au baridi kali, huweza kusababisha mafua makali ambayo huambukiza, kuongezeka kwa ukali wa vimelea wa kuleta ugonjwa mfano kutokea kwa virusi vipya ambavyo watu hawana kinga nayo bado, kufika kwa virusi katika mazingira mapya n.k.
Kufuatia kutokea kwa mlipuko wa ugonjwa wa Ebola nchini Tanzania, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupitia kwa Waziri mwenye dhamana Mhe. Ummy Mwalimu mnamo tarehe 28 Septemba, 2022 ilitoa taarifa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari na kusema kuwa mlipuko wa Ugonjwa huo nchini Uganda unaiweka nchi yetu katika hatari kubwa kutokana na muingiliano mkubwa wa shughuli za kiuchumi na kijamii kupitia mipaka rasmi na isiyo rasmi.
Taarifa hiyo ilifafanua zaidi kuwa Mikoa iliyo hatarini zaidi kupata ugonjwa huo ni Kagera, Mwanza, Kigoma, Geita na Mara. Aidha Mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Kilimanjaro, Songwe, Mbeya na Dodoma ipo katika hatari kwa sababu ya uwepo wa viwanja vya ndege na vituo vikubwa vya mabasi ya kutoka nchi jirani.Hata hivyo, hadi sasa hakuna mgonjwa wa Ebola nchini Tanzania .Hivyo kila mmoja ametakiwa kuchukua tahadhari na kuhakikisha ugonjwa huo hauingii nchini.
Kutokana na wito huo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kupitia Idara ya Afya imejitahidi kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kutoa elimu kwa wananchi juu ya hatua mbalimbali za kuchukua ili kujikinga na magonjwa ya mlipuko .Mbali na utoaji wa elimu imefanikiwa kujenga jengo au wodi katika eneo la Kipawa ambalo mpaka sasa limegharimu fedha kiasi cha Shilingi Milioni 368 ambayo ni fedha kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji, jengo hilo litaweza kupokea wagonjwa wa magonjwa yote ya mlipuko ikiwepo kipindupindu ,Ebola, UVIKO 19 n.k. endapo watatokea.
Wodi ya magonjwa ya milipuko iliyopo Kipawa |
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambaye ndiye Mkuu wa Idara ya Afya Dkt. Elizabeth Nyema, amesema kuwa kwa sasa jengo hilo lipo tayari kupokea wagonjwa na timu ya wataalamu wamekwishapatiwa mafunzo hivyo wapo tayari kutoa huduma kwa wagonjwa wakati wowote watakapohitajika.Ameongeza kuwa wao kama wataalamu wanafanya kazi kwa kushirikiana na watoa huduma ngazi ya Jamii ambapo wataalam hao wana wajibu wa kutoa elimu na kuhamasisha katika maeneo yao mara kwa mara lengo likiwa ni kuhakikisha jamii inaelewa nini maana ya magonjwa ya mlipuko, viashiria vya mgonjwa aliyepata maambukizi mapya na njia mbalimbali za kujikinga.
Dkt. Nyema pia ameeleza kwa kifupi kuhusiana na Jiografia ya jengo hilo kuwa litakuwa na uwezo wa kuchukua wagonjwa wapatao 25 ambapo wodi zimetenganishwa kutokana na maelekezo ya kitaalamu ambapo kuna wodi kwa ajili ya wagonjwa ambao ni wahisiwa na wodi ambayo ni kwa ajili wa watu waliothibitika kuwa na maambukizi tayari.
Aidha amebainisha kuwa Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam haijaishia hapo katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko. Matarajio yao ni kuendelea kujenga vituo vingine katika maeneo mengine. Mfano ndani ya ramani ya Hospitali ya Wilaya ya Kivule kuna eneo limetengwa kwa ajili ya kujenga jengo la magonjwa ya mlipuko. Hivyo katika bajeti ijayo wanatarajia kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi ya jengo hilo kwa ajili ya wanawake na wanaume kwa sababu eneo la Kipawa lina uwezo wa kupokea wagonjwa wachache. Hivyo wao kama wataalamu wameona lazima wachukue tahadhari ya kuwa na vituo vya ziada endapo watatokea wagonjwa katika kituo cha Kipawa na wakazidi uwezo wa kituo, pawepo na eneo jingine la kuwapeleka.
Wito umetolewa kwa wananchi kuwa na mwitikio chanya pale elimu inapotolewa kuhusiana na magonjwa ya mlipuko. Ili kuepukana na magonjwa hayo jamii imetakiwa kufanya usafi wa mazingira kwa wakati na mara kwa mara. Pia kukusanya na kutupa takataka katika maeneo yaliyotengwai, kunawa mikono wakati wote, sababu maambukizi ya magonjwa ya mlipuko yanaambukizwa kwa kushikana mikono au kukutana na kinyesi au mkojo ambao tayari una maambukizi. Hivyo ili tuwe salama zaidi inatupasa tuchukue tahadhari hizo na tufuate ushauri na maelekezo yote tunayopewa na wataalamu wa afya.