Waziri Kairuki akagua Miradi ya Maendeleo Jimbo la Ukonga

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Angellah Kairuki ametoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuhakikisha wanalipa fidia katika eneo la ekari 2.7 lililochaguliwa kwaajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Kitunda Relini ili ujenzi huo uweze kuanza kwa wakati huku pia akiwapa siku Saba za kuhakikisha Nyaraka za Soko la Kivule zinakamilika kuandaliwa na kutumwa katika ofisi za OR-TAMISEMI.


Mhe. Kairuki ametoa maelekezo hayo leo Februari 23, 2023 wakati wa Ziara yake aliyoifanya katika Jimbo la Ukonga lengo likiwa ni kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Halmashauri hiyo hususani katika miradi ya Elimu, Afya, Miundombinu ya barabara pamoja na kufanya mkutano wa hadhara na wananchi wa Jimbo la Ukonga.


Aidha Mhe. Kairuki amesema "Niwapongeze kwa kukubali kulipa fidia takribani kiasi cha shilingi million 387 kwa ajili ya eneo la kujenga shule ya Sekondari Kitunda Relini, hivyo fedha hizo zilipwe kwa wakati na tufuate sheria kanuni na taratibu za malipo kwa kuzingatia maelekezo ya mthamini wa Serikali, fedha hizo zilipwe kwa ukamilifu wake na nyaraka zote zihifadhiwe"

Sambamba na Hilo Mhe. Kairuki ameeleza kuwa kiasi cha shilingi bilioni 1.2 zimetengwa kwaajili ya miradi wa mpango wa kuboresha elimu ya Sekondari (Secondary Education Quality and Improvement Programme (SEQIP) ambazo zitatumika katika kutekeleza mradi wa ujenzi wa Shule mbili (2) za Sekondari ikiwemo Shule mpya ya Sekondari Kitunda Relini pamoja na Shule mpya ya Sekondari Msongola.


Mheshimiwa Kairuki amesema “Baada ya taratibu za kulipa fidia kukamilika kiasi cha fedha takribani shilingi millioni 600 kitatolewa katika ujenzi wa Shule ya Sekondari Kitunda Relini ambapo kiasi cha shilingi millioni 470 kitatolewa kama malipo ya awali kwa ajili ya kujenga vyumba nane (8) vya Madarasa, jengo la TEHAMA, jengo la Utawala, Maktaba, vyumba vitatu(3) vya maabara ya Fizikia, Kemia, na Biolojia pamoja na matundu ya vyoo hivyo baada ya kukamilisha hayo tutakagua na tukiridhishwa na ujenzi huo tunatoa shilingi milioni 130 ambapo milioni 100 itatumika kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu na milioni 30 zitatumika kununulia vifaa kwa ajili ya jengo la TEHAMA vivyo hivyo tutafanya katika shule mpya ya Sekondari Msongola"

Aidha katika ziara hiyo Mheshimiwa Kairuki aliweza kutembelea miradi ya ujenzi wa barabara zinazojengwa kwa kiwango cha Lami inayotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ikiwemo barabara ya Banana-Kitunda-Kivule-Msongola ya Km 14.7 pamoja na Barabara ya Chanika - Homboza ya Km 4.54 ambapo kwa upande wa barabara ya Km 14.7ambayo kwa muhimu wake barabara hii ilipendekezwa iingizwe katika mpango wa DMDP Phase II, lakini pia Halmashauri imeweza kutenga kiasi cha shilingi milioni 800 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kujenga km 0.5 na pia kwa mwaka wa fedha 2023/2024 zimetengwa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kujenga urefu wa km 1.0 huku Barabara ya Banana -Chanika inayounganisha Wilaya ya Ilala na Kisarawe ya Km 4.54 kwa Bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 iliweza kutengwa fedha kiasi cha shilingi bilioni 6.65 kutoka kwenye TOZO kwa ajili ya kukamilisha mradi huo ambao upo chini ya Mkandarasi Esteem Construction Limited naumefikia asilmia 40% hivyo hadi kufikia Julai 20, 2023 mradi huo utakua umekamilika.


Akiendelea na ziara hiyo katika kituo cha Afya Chanika Mheshimiwa Kairuki amefurahishwa na huduma zinazopatikana humo na kuwahakikishia ataendelea kutatua changamoto ndogondogo za upungufu wa wataalamu, Ujenzi wa ghorofa, ukosefu wa maji ya DAWASA pamoja na upungufu wa gari la kubebea wagonjwa (Ambulance). “ Kituo hiki kimekua muhimu sana kwa wananchi wa Chanika hivyo tutatoa gari la kubebea wagonjwa (Ambulance) itakayotumika kwa ajili ya rufaa za kituo hiki pia kwa upande wa kuongeza Wataalamu wa Afya pamoja na ujenzi wa ghorofa maelekeza kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la DSM kuona namna gani watatumia mapato ya ndani kuajiri Wastaafu kwa mikataba ambao bado wana nguvu za kufanya kazi pamoja na kuhakikisha wanatao fungu lingine kuanza ujenzi wa ghorofa na Baadaye sisi kama Serikali tukipanga bajeti ya kutenga fedha za kukamilisha jengo hilo kusudi wananchi wetu waendelee kupata huduma bora na za uhakika kwa wakati.” Amesema Mhe.Kairuki.

Sambamba na hilo Mhe. Kairuki ameweza kutembelea Shule ya Msingi ya Mikongeni kujionea ujenzi wa madarasa mawili ya Mfano yaliyojengwa kwa kiasi cha shillingi million 55.8 kwa ajili ya watoto wa awali wa shule hiyo kusoma katika mazingira bora na rafiki ili kuweza kuongeza ufaulu na kuboresha elimu ya Msingi.


Naye Mbunge wa Jimbo la Ukonga Mhe. Jerry Silaa amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu kwa kujali wananchi wa Jimbo la Ukonga kwa kutoa fedha katika kutekeleza miradi mbalimbali ya Maendeleo ikiwemo kwenye Sekta ya Afya, Elimu pamoja na Barabara. Pia ampongeza Waziri OR-TAMISEMI Mhe. Angela Kairuki kufanya ziara ya kutembelea miradi iliyopo ndani ya Jimbo la Ukonga ambayo imetekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kupitia mapato yake ya ndani na fedha toka kwa Mhe. Rais Dkt. Samia sambamba kusikiliza wananchi wa Jimbo la Ukonga.


Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo amemuhakikishia Waziri OR-TAMIISEMI Mhe. Kairuki kwamba watafuata maelekezo yote yaliyoelekezwa na Serikali.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi