RC DSM aridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na Jiji la DSM

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila aridhishwa na matumizi ya fedha na kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kupitia fedha toka Serikali Kuu pamoja na fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri.


Hayo ameeleza leo tarehe 28 Juni, 2023 Jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimlbali ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa mwaka 2022/2023 lengo likiwa ni kuhakikisha Ilani ya Chama cha Mapinduzi inatekelezwa kwa kasi zaidi.


Miradi iliyotembelewa na Mkuu wa Mkoa ni pamoja na ukamilishaji wa ujenzi wa madarasa ya ghorofa 5 katika shule ya Sekondari Liwiti itakayogharimu takribani shilingi bilioni 1.57 pindi likikamilika, ukaguzi wa ujenzi wa Shule Mpya ya Msingi Kivule Mpya yenye madarasa 14 na matundu 16 ya vyoo ambapo ujenzi huo upo hatua ya umaliziaji na hadi kufikia Juni 30, 2023 ujenzi unatarajiwa kukamilika na utagharimu takribani shilingi milioni 475.3 zikiwa ni fedha kutoka mradi wa Boost pamoja na ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Zingiziwa wenye thamani ya shilingi milioni 500 zikiwa ni fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri.


Akizungumza na wananchi baada ya kukagua mradi Mhe. Chalamila alisema ili kuacha alama Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan aliamua kuwekeza nguvu zaidi katika sekta ya elimu na Afya ili wananchi wapate huduma bora kwa ukaribu zaidi na kwa wakati.

Napenda kuwapongeza viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa ufuatiliaji na usimamizi mzuri wa miradi kwani kupitia miradi hii changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi zitakuwa zimetatuliwa kwa kiasi kwani mmejengewa vituo vya afya pamoja na shule maeneo ya Karibu zaidi hivyo naamini ukaribu wa huduma hizi utapunguza adha mbalimbali zikiwemo toro kwa wanafunzi pamoja na vifo vya uzazi, niwaombe mtumie vizuri rasilimali hizi na kwa changamoto ndogondogo tutaendelea kuzitatua na mambo yatakua mazuri zaidi." Ameeleza Mhe. Chalamila.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo ametoa shukurani zake kwa Mkuu wa Mkoa kwa Ziara aliyoifanya ya kukagua miradi ya Maendeleo pamoja na kuongea na wananchi huku akimuhakikishia kutekeleza yote aliyoyaagiza.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi