Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama (Mb), amewataka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) kuimarisha kivuko cha Mwanagati-Magole mara tu baada ya mvua kupungua.
Waziri Mhagama ameyasema hayo leo Novemba 22, 2023 alipokuwa akiongea na wananchi wa Mtaa wa Mwanagati na Magole katika ziara yake ya kufanya tathmini na ufuatiliaji wa maeneo yaliyoathiriwa na mvua kwa Mkoa wa Dar es Salaam ambapo eneo mojawapo likiwa ni eneo la daraja linalounganisha Mitaa hiyo ya Kata ya Mzinga Jijini Dar es Salaam.
“Agizo la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha miundombinu yote yahuduma kutoa huduma kwa wananchi wa Tanzania na ndio maana kutokana na umakini wa Serikali yetu leo tumefika mahali hapa kujionea wenyewe adha wanayoipata wananchi wa Kata ya Mzinga hivyo tumetoa shilingi milioni 20 kwa ajili ya TARURA kuimarisha kivuko hiki hivyo niwaombe wataalamu kutoka TARURA mara tu baada ya mvua kupungua kivuko hiki kiimarishwe ili wananchi waweze kupita muda wote huku mipango ya kujenga kivuko cha muda mrefu ikiendelea kufanyika kwani mvua zikiisha kivuko cha muda mrefu kitaaza utekelezaji, pia nitoe angalizo fedha hizi zitumike ipasavyo isitokee mtu yoyote kuweka mfukoni mwake kwani hatua za kisheria zitachukuliwa na pindi tu mtakapoanza ujenzi wananchi washirikishwe kwa ukaribu zaidi katika hili,” Amesema Mhe. Mhagama.
Akiendelea kuongea na wananchi wa Kata ya Mzinga Mhe. Mhagama ametoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari kipindi hichi cha mvua hasa wale wanaoishi karibu na mikondo ya maji huku akiwasisitiza kutunza mazingira kwa kuyaweka katika hali ya usafi ili kuepukana na magonjwa ya mlipuko kama Kipindupindu ambayo hutokea kipindi hiki cha mvua.
Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila ameema “Tunaishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuja kuona hali halisi ya namna ilivyo lakini nipende kuwaambia mpaka sasa Dar es Salaam hakuna mafuriko bali kwa wananchi wa Mzinga adha yao kubwa ni miundombinu ya Daraja pamoja na miundombinu ya barabara ambayo imeharibiwa na mvua hivyo niwahakikishie adha hii inakwenda kuisha kwani tayari TARURA wameshachora mchoro wa kujenga daraja hili ambao utagharimu shilingi bilioni 1.7 lakini pia kwa upande wa barabara DMDP awamu ya pili barabara hii imeingia kwenye mradi huu hivyo itatengenezwa barabara ya kiwango cha lami yenye KM 7 itakayoka kwa Mpalange Mpaka kuunganisha barabara ya Mwanagati inayopitia Banana hivyo niwaombe mume wavumilivu kwani kero zenu tumezisikia na tunazifanyia kazi.”
Awali akiongea wakati wa ziara hiyo Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo Ametoa shukrani zake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuhakikisha Wananchi wanapata huduma kwa wakati huku akimuhakikishia Waziri Mhagama kusimamia kwa ukaribu zaidi yote atakayoyaelekeza.