Shirika la Ushirikiano wa Elimu Duniani (GPE) laahidi kushirikiana na Tanzania katika kuboresha Sekta ya Elimu

Shirika la Ushirikiano wa Elimu Duniani (GPE) laahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuboresha sekta ya elimu Nchini, hayo yamebainishwa leo Desemba Mosi na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa GPE, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa GPE, Bi. Laura Frigenti wakati wa ziara yao ya kutembelea shule ya Msingi Mikongeni iliyoko Gongo la Mboto Jijini Dar es Salaam lengo likiwa ni kukagua miradi ambayo GPE imechangia kwenye shule hiyo.


Akiongea wakati wa ziara hiyo Dkt. Kikwete ameeleza kuwa “Shirika la Ushirikiano wa Elimu Duniani ni wadau wetu muhimu sana kwenye kuhakikisha sekta ya elimu inakua kwa kasi nchi kwani kupitia shirika hili toka mwaka 2013 tulipoingia makubaliano nao Serikali ya Tanzania tumeweza kupokea Dola milioni 332 kwaajili ya kuendeleza sekta ya elimu, kuchapisha na kusambaza vitabu vya kiada milioni 10 Shuleni, hata hivyo tayari GPE imetia saini na Serikali, makubaliano ya kutoa dola milioni 80 (zaidi ya shilingi Bilioni 201) kwaajili ya kusaidia mafunzo ya walimu nchini hivyo nimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali ushirikiano huu pamoja na kuridhia kikao kifanyike nchini Tanzania ambapo Mimi kama Mwenyekiti wa GPE nitaongoza vikao vya Bodi vya Shirika hilo huko Zanzibar tarehe 4 hadi 6 Disemba ikiwa ni mara ya kwanza kwa Shirika hilo la kimataifa kufanya vikao vyake vya bodi barani Afrika.


Sambamba na hilo Dkt. Kikwete ameendelea kusema GPE itaendelea kusimama na Tanzania ili kuhakikisha elimu ya Tanzania inaendelea kukua kwa kasi pamoja na kuhakikisha haki kwa kila mwanafunzi huku akisisitiza fedha zinazotolewa na GPE kwaajili ya kuboresha miundombinu ya elimu zitumike kama inavyotakiwa.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa GPE Bi. Laura Frigenti ameeleza kuwa wao kama GPE wanafuraha kubwa kuja Tanzania kukagua miradi yao huku akisisitiza kuwa ushirikiano wa GPE na Tanzania ni wa muda mrefu na utasaidia watoto wadogo kupata elimu kwaajili ya kutimiza ndoto zao.


Naye Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb) amesema kuwa “Nipende kutoa shukrani zangu kwa Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete pamoja na GPE wote kwa ujumla kwa kutembelea Tanzania kujionea miradi yenu na jitihada mnazozionesha kuhakikisha sekta ya elimu nchini inakua kwa kasi.

Awali akitoa taarifa kwa wageni hao Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mikongeni Mwl. Saimon Mndendemi ameeleza kuwa kupitia shirika la GPE shule imepokea shilingi milioni 55. 8 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili ya awali pamoja na matundu 6 ya vyoo ambayo yameweza kuwa mchango mkubwa kwa shule kwani wanafunzi wanasoma katika mazingira mazuri na rafiki, pia ameshukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta mradi huo shule ya mikongeni hivyo wanaahidi kuyatunza madarasa hayo ili yaweze kudumu kwa muda mrefu.


Ikumbukwe kuwa GPE ni Shirika lililolenga kusaidia nchi zinazoendelea ili watoto waweze kupata elimu bora huku wakitoa kipaumbele kwenye elimu ya mtoto wa kike ambapo katika nchi 180 za GPE Tanzania ikiwa mojawapo.


Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi