Wananchi watakiwa kujitokeza kwa wingi kwenye Ardhi Klinic

Kamishna wa Ardhi Msaidizi wa Mkoa wa Dar es Salaam Ndg. Shukrani Kyando amewataka Wananchi wa Jiji la Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kupata huduma kwenye 'Ardhi Klinic' iliyoandaliwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

Kyando ametoa rai hiyo Leo tarehe 16 Desemba, 2023 katika viwanja vya Nguvu Mpya vilivyoko katika Kata ya Chanika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

Aidha ameongeza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza kuwasogezea wananchi huduma muhimu kwenye maeneo yao, hivyo katika kutekeleza hilo wameanzisha zoezi la Ardhi Klinic ambapo wataalamu wa Ardhi watakuwa wakiwafuata wananchi katika maeneo yao na kutatua changamoto zao zinazohusiana na masuala ya Ardhi ikiwemo kutoa elimu kuhusiana na Ardhi, kusikiliza na kutatua migogoro ya Ardhi, Kuandaa na kutoa hati miliki, Taratibu za kupata vibali vya ujenzi na huduma nyingine nyingi.

Naye Paulo Kitosi kutoka Timu ya Uratibu mradi wa Uboreshaji, Usalama wa milki za Ardhi nchini amesema kuwa zoezi hili limeanzishwa kwa nia ya kukwamua urasimishaji Ardhi uliokwama kwa kutoa hati za Ardhi papo hapo na kukwamua Upimaji ambao haujakamilika.

Amesema, "Serikali imeanzisha zoezi hili ili Ardhi iweze kupimwa na kupangwa rasmi lengo ikiwa ni kuondoa migogoro ya Ardhi iliyokuwepo.Vilevile wananchi waweze kupata hati miliki na kuwa na usalama wa umiliki wa Ardhi."

Serikali ya awamu ya sita ambayo inaongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ilibuni mradi huu wa Ardhi Klinic ambapo wataalamu wa Ardhi watatoa huduma kwa wananchi wa kuwafuata mahali walipo.

Kwa upande wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam zoezi hili linatarajiwa kufanyika kwa muda wa siku 25.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi