DC Mpogolo azindua vyumba vya madarasa Shule ya Sekondari Vingunguti

Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo Leo Januari 16, 2024 amezindua vyumba viwili (2) vya madarasa ya kisasa, Ofisi ya Mkuu wa Shule pamoja na matundu kumi na mbili (12) ya vyoo katika Shule ya Sekondari Vingunguti yaliyojengwa na wadau Mohamed Builders Investment pamoja na kuzindua vivuko kumi (10) vilivyojengwa kwa gharama ya Shilingi Milioni 13.9 ndani ya Kata ya Vingunguti.


Akiongea na wananchi na wanafunzi wa shule hiyo amesema "Kipekee napenda kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mstari wa mbele katika kuboresha sekta ya Elimu nchini. Madarasa haya yamejengwa kutokana na mahusiano mazuri aliyonayo Mhe. Rais na wadau mbalimbali wa sekta ya Elimu. Pia Mhe. Rais ametoa fedha kwaajili ya ujenzi wa jengo la ghorofa tano (5) litakalokua na madarasa kumi na sita (16) ujenzi ambao unatarajiwa kuanza mwezi Februari."


Sambamaba na hilo, Mhe. Mpogolo amewaasa wazazi na walezi kuhakikisha wanawapeleka watoto shule kwani elimu kuanzia ngazi ya awali mpaka Sekondari ni bila malipo.


Aidha, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam Ndg. Ally Bananga ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kusimamia miradi kwa ufanisi na kuwasihi kuhakikisha thamani ya pesa inayotolewa na Mhe. Rais inatumika ipasavyo kwa lengo la kuleta maendeleo kwa wananchi.


Awali akisoma risala kwa mgeni rasmi, Mkuu wa Shule hiyo Mwl. Wendo Mwalyusi amesema licha ya shule yake kuwa na mafanikio kwa zaidi ya miaka 10, kumekua na upungufu wa walimu wa sayansi hivyo kupelekea shule kutumia fedha za miradi ya shule kuajiri walimu wa muda (part time) na kushindwa kufanya mambo mengine ya maendeleo ya shule na kumuomba Mkuu wa Wilaya kuwasilisha jambo hilo kwa mamlaka husika.


Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi