RC awataka wananchi wanaoishi maeneo hatarishi kuchukua tahadhari

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila amewataka wananchi wa Kata ya Vingunguti na Mkoa wa Dar es Salaam kiujumla kuchukua tahadhari mapema ya mvua zinazoendelea kunyesha kabla athari hazijatokea.


Hayo ameyaeleza leo Januari 10, 2024 alipokua akiongea na Wananchi wa Mtaa wa Butiama, Kata ya Vingunguti wakati wa ziara ya kukagua maeneo yaliyoathirika na mvua zinazoendelea kunyesha.


RC Chalamila amesema “Rais ameshaanza kufanya maboresho ya Mto Msimbazi na wananchi mnaoishi karibu na mto huo mnatakiwa kuhama ili marekebisho makubwa yafanyike. Msione kama Serikali inawaonea ila tupo kwaajili ya kunusuru maisha yako na kizazi chako pamoja na mali zenu hivyo ni muhimu kuchukua hatua kwa yale maeneo hatarishi."

Sambamba na hilo, Mhe. Chalamila ametoa maelekezo kwa Mamlaka ya Bonde kutoa vibali vya dharura vya usafishaji wa Mito kwa watu binafsi wenye mitambo ya uhakika ya kusafisha mito ili waweze kusaidia na kuzuia athari zinazotokana na kujaa kwa Mto Msimbazi.


Aidha Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo amemshukuru Mkuu wa Mkoa na kumuahidi kutekeleza yale yote aliyomuagiza ili kunusuru makazi na miundombinu.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi