Waziri Mchengerwa awaagiza Wakuu wa Mikoa kufanya uwiano wa walimu mashuleni

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa ametoa maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa kufanya uwiono sawa wa walimu katika shule zote za Serikali.


Hayo ameyaeleza leo Januari 8, 2024 alipotembelea shule ya Sekondari Benjamin Mkapa kwenye ziara ya kukagua mapokezi ya wanafunzi wapya wa kidato cha kwanza kwa muhula wa kwanza kwa mwaka 2024 pamoja na kukagua ujenzi wa maktaba pamoja na kiwanja cha mpira.


Akizungumza na wanafunzi katika shule hiyo Waziri Mchengerwa amesema "Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anadhamiria kuifanya sekta ya elimu iwe sawa katika maeneo yote nchini. Lengo ni kutaka shule za Serikali kuwa bora kuliko shule binafsi, hivyo niwaombe Wakuu wa Mikoa yote kusimamia na kuhakikisha kunakua na uwiano sawa wa walimu katika shule zote kulingana na wanafunzi waliopo shuleni, ili wanafunzi wetu waweze kupata elimu sawa."


Sambamba na hilo Mhe. Mchengerwa amesema “Rais ametoa kiasi Cha shilingi bilioni 33.3 kwa ajili ya elimu bure kote nchini, hivyo niwatake wazazi wenye watoto waliofaulu kuwaleta shuleni kwani walimu wako tayari kutoa elimu ambayo Mhe. Rais ameikusudia. Pia nawasihi wanafunzi mlioanza kidato Cha kwanza kuhakikisha mnasoma kwa bidii ili kuzifikia ndoto zenu"


Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila amemshukuru Waziri Mchengerwa kwa kutembelea shule ya Sekondari Benjamin Mkapa. Pia amesema "Shule hii ni moja ya shule kubwa nchini na ina wanafunzi wengi lakini inakabiliwa na changamoto ya kutokua na gari la dharura pale kunapotokea shida kwa wanafunzi hivyo nakuomba utufikishie ombi letu kwa Waziri wa Fedha ili tupate gari kwa ajili ya dharua shuleni hapa."

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi