Maafisa Ugani wakabidhiwa Pikipiki

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila leo tarehe 7 Machi, 2024 amekabidhi pikipiki ishirini na nne (24) aina ya Boxer zilizotolewa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Maafisa Ugani wa Halmashauri za Mkoa wa DSM ambazo zitarahisisha utendaji kazi.


Akikabidhi pikipiki hizo zenye jumla ya thamani ya Tsh. Milioni 72, Mhe. Chalamila amewataka kwenda kuzitunza na kuzifanyia kazi iliyokusudiwa ambapo amesema pikipiki hizo zitawasaidia kurahisisha usafiri katika maeneo yao ya kazi ikiwa ni jitihada ya kuhakikisha wanawafikia wafugaji na kutatua changamoto zinazowakabili.


"Pikipiki hizi zikafanye kazi iliyokusudiwa ambayo ni kuwafikia wakulima kwenye maeneo yao na kuwapa elimu huku mkizingatia Sheria za Usalama barabarani mnapoendesha vyombo hivyo vya moto. Vilevile zikawasaidie kufanya ukaguzi wa viwanda na maduka ya kuuzia vyakula vya mifugo, kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao ya mifugo pamoja na kurahisisha udhibiti wa magonjwa ya mifugo." Amesema Mhe. Chalamila.


Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la DSM akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la DSM Ndg. Merchades Rusasa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwafikia Wananchi wa Ilala katika Sekta ya Kilimo na kuwataka Maafisa Ugani hao kutumia pikipiki hizo kuwatembelea Wakulima, Wafugaji na Wavuvi ili kutoa elimu na kutatua changamoto zinazowakabili pamoja kutoa huduma bora za ugani, kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao na mifuyo pamoja na kutoa elimu bora kwa wakulima.


Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi