Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kupitia Kitengo cha Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira leo tarehe 7 Machi, 2024 imetoa elimu ya kutumia nishati safi na kusitisha matumizi ya mkaa na kuni kwa mama na baba lishe wa Soko la Kisutu.
Akiongea wakati wa utoaji wa elimu hiyo, Afisa Mazingira Ndg. James Mduma amewaasa mama na baba lishe hao kuacha kutumia mkaa na kuni kwani huzalisha kiwango kikubwa cha hewa ya ukaa (kabonidioksidi) ambayo huchangia kwa kiasi kikubwa katika uharibifu wa Mazingira unaopelekea kuongezeka kwa madhara yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi.
"Kuni na mkaa zina madhara mengi kwa binadamu na mazingira. Husababisha upotevu wa bioanuwai maeneo ya Vijijini na Mijini pamoja na kusababisha ongezeko la joto. Kwa kuacha kutumia kuni na mkaa, itasaidia kuokoa muda unaopotea kwa kutafuta kuni na kuongeza muda wa uzalishaji kwa hivyo kuongeza kipato." Amesema Ndg. Mduma.
Itakumbukwa Aprili 19, 2023 Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) ilitoa katazo kwa taasisi za umma na binafsi kuacha kutumia kuni na mkaa na badala yake kutumia nishati mbadala ili kupunguza kasi ya ukataji wa miti ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoathiri mazingira na uchumi.